Maelfu ya wakazi wa jiji la Mbeya jana walifurika katika viwanja vya Ruanda Nzovwe kumsikiliza mgombea urais kupitia Chadema na Ukawa, Edward Lowassa aliyefika jijini hapo kutafuta wadhamini.

Lowassa alilakiwa na wakazi wa jiji hilo katika uwanja wa ndege wa Songwe na kumsindikiza hadi katika viwanja hivyo huku mamia wakazi wengine wakijipanga barabarani hadi katika uwanja huo.

Akiwahutubia wananchi hao, Lowassa ambaye aliambatana na mgombea mwenza Juma Haji Duni na wenyeviti wa Ukawa, aliwaahidi wakazi wa jiji hilo kuwa endapo atachaguliwa, atahakikisha jiji hilo linakuwa jiji la kimataifa kama ilivyo nchi ya Swaziland inayozungukwa pande zote na Afrika Kusini.

Mgombea huyo wa Ukawa aliwahakikishia wananchi hao kuwa katika harakati za kulifanya jiji hilo kuwa la kimataifa, atahakikisha uwanja wa ndege wa Songwe unakuwa uwanja wa kimataifa.

Katika ahadi nyingine, Lowassa alieleza kuwa atahakikisha anawainua wakulima na kuboresha ujira za wafanyakazi mazingira ya kazi kwa ujumla.

Alisisitiza kuwa ataunda baraza la mawaziri wachapakazi watakaofanya kazi muda wote huku akitoa onyo kwa wale watakaotaka kuhujumu sekta ya kilimo kwa kuchelewesha pembejeo kwa wakulima kuwa watakaofanya hivyo watakiona cha moto.

Lowassa ambaye ni waziri mkuu wa zamani, aliahidi kuwa serikali yake itaendeshwa kwa mwendo wa mchakamchaka.

Safari ya Lowassa ilikuwa ya mafanikio katika jiji hilo kwa kuwa alipata zaidi ya wadhamini 50,000.

Ukawa: Amri Ya Polisi Kuzuia Maandamano Haituhusu
Wizkid Kufanya Remix Ya Wimbo Wa AY