Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amezungumzia kilichojiri katika mkutano Mkuu wa CCM baada ya wajumbe wengi kuimba ‘tunaimani na Lowassa’ baada ya jina lake kukatwa katika mchakato wa kumpata mgombea urais wa chama hicho mwaka jana.

Lowassa ameeleza kuwa hakufahamu kama wajumbe hao wangechukua hatua hiyo wakati huo hivyo kwake ilikuwa kama surprise.

Lowassa ambaye hivi sasa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema, alisema kuwa hatua hiyo ilimaanisha wananchi kueleza walichokitaka hata kama viongozi wa walikuwa hawakubaliani nacho.

“Ile ilikuwa inaexpress watu walichokuwa wanataka. Inawezekana msikubaliane na walichokuwa wanaexpress lakini waliexpress wanachokata,” Lowassa alifunguka katika kipindi cha ‘Funguka’ cha Azam TV.

Hata hivyo, Lowassa ambaye baadae alishiriki kuyapigia kura majina matano yaliyokuwa yamebakizwa katika kinyang’anyiro hicho cha kumpata mgombea urais wa CCM alitakaa kumtaja chaguo lake kati yao akieleza kuwa itabaki kuwa siri yake.

Akizungumzia urafiki wake na Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete ambao uliingia dosari tangu mwaka 2008 na hatimaye kukata jina lake katika kinyang’anyiro hicho cha urais, alisema kuwa hana tatizo naye na kwamba hataki kumhukumu bali ajihukumu yeye mwenyewe na wananchi.

Mwanasiasa huyo mkongwe alieleza kuwa ana furaha kura Chadema na hajutii uamuzi wa kuihama CCM, huku akisisitiza kuwa anaamini atashinda katika uchaguzi mkuu ujao endapo utafanyika kwa uhuru na haki.

 

Video: Aje ya Ali Kiba yafanyiwa 'remix' Kenya
Serikali kuwaondoa Wakurugezi Watakaotoa taarifa za uongo