Waziri Mkuu wa zamani na mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, Edward Lowassa amekosoa hatua za kukamatwa kwa viongozi wa chama hicho waliochaguliwa na wananchi na kuiomba kamati kuu ya chake hicho kuvijadili na kutoa maamuzi.
Lowassa alizungumzia matukio hayo wakati wa kushiriki ifutar iliyoandaliwa na madiwani wa Chadema na viongozi wengine wa chama hicho, iliyofanyika Mikocheni jijini Dar es Salaam.
“Hili ni lazima lijadiliwe kwenye kikao [cha Kamati Kuu] na uamuzi tutakaouchukua tuwashirikishe wananchi wetu. Na baada ya hapo tuseme imetosha na tuchukue hatua,” alisema Lowassa.
“Kitendo cha kuwakamata viongozi wetu waliochaguliwa sio kizuri, kinawadhalilisha. Na hili halikufanyika Ubungo tu, hata Arusha pia limefanyika. Hatuwezi kuruhusu jambo hili likaendelea, na kama likiendelea ni makosa,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, mwanasiasa huyo alisema kuwa katazo la kutofanya mikutano ya kisiasa hadi 2020 pia linapaswa kuangaliwa upya na chama hicho kwani viongozi wa CCM wanazunguka na kuzungumza na wananchi.
Hivi karibuni, baadhi ya viongozi wa Chadema ikiwa ni pamoja na meya wa Ubungo, Boniface Jacob walikamatwa na jeshi la polisi kwa amri ya mkuu wa wilaya, wakidaiwa kuwa kabla ya ziara yao waliyopanga kukagua miradi walifanya mkutano wa chama katika jengo la Serikali.