Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita jana lilimkamata na kumfikisha kituoni waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kabla ya kumhamishia kwenye ofisi ya Kamanda wa Polisi na baadae kuachiwa.

Taarifa kutoka mkoani humo zimeeleza kuwa Lowassa ambaye yuko mkoani humo kwa ajili ya kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Mkome, alichukuliwa na Jeshi la polisi baada ya kuingia katika soko kuu la Geita kwa lengo la kuwasalimia wananchi.

Lowassa alielekea katika kituo cha polisi baada ya kuamriwa na askari polisi waliofika katika eneo la soko hilo wakiwa kwenye magari mawili ya jeshi hilo.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo aliwaambia waandishi wa habari kuwa jeshi hilo halikumkamata Lowassa bali lilifanya nae majadiliano kuhusu usalama wake kwa kuingia ndani ya soko hilo.

“Tulijaribu sana kuelezana na kuelimishana katika eneo zima la usalama na ulinzi kwa ujumla. Kwahiyo ukiangalia hata nafasi yake kidogo ni kubwa. Kwahiyo tuliona pia kuwa sisi tuna jukumu la kuona pale ambapo kuna matatizo ya ulinzi na usalama kwa ujumla, kwake yeye binafsi na jamii,” Mponjoli Mwabulambo.

Lowassa ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, yuko mkoani Geita akiwa ameongozana na baadhi ya viongozi wa kitaifa wa chama hicho kama Profesa Mwesiga Baregu, Hamisi Mgeja, na mwenyeji wao ambaye ni mbunge wa viti maalum Upendo Peneza (Chadema).

Kongo Ya Kabila Yawaliza Morocco
#HapoKale