Ndoto ya kuingia Ikulu bado inaendelea kuwaka kichwani kwa aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa.

Lowassa ameeleza kuwa bado anaamini ataingia ikulu siku moja kwa kuwa anaamini ndiye aliyekuwa mshindi katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Okotoba 25 na kwamba serikali ya awamu ya nne kwa kushirikiana na CCM walichakachua kura zake.

Waziri Mkuu huyo wa zamani aliyasema hayo jana jijini Arusha wakati akimnadi mgombea ubunge wa jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema.

“Naomba niwaambie nawapenda sana Watanzania sihitaji kuingia ikulu kwa damu ya watu. Naamini Watanzania hawa hawa watanipeleka Ikulu siku moja, bado nipo imara,” alisema Lowassa ambaye alikuwa anashangiliwa muda wote na wafuasi wa chama hicho waliohudhuria.

“Hawa CCM na serikali wamechakachua kura zetu, dunia inajua. Naomba niwahakikishieni tumeshinda uchaguzi mkuu, sisi ndiyo washindi hata wao wanajua. Tembeeni kifua mbele sisi ni washindi,” aliongeza.

Aliwataka wananchi wa Arusha kuwa watulivu wakati wote ili wasiipe serikali sababu ya kutumia magari ya washawasha aliyodai yameigharimu nchi dola milioni 200. Alisema kuwa hivi sasa polisi wanatafuta namna ya kuyatumia ili wapate sababu ya kuhalalisha manunuzi ya magari hayo.

Magufuli ataja Baraza lake la Mawaziri, Orodha ya wateuliwa iko hapa
Wimbo Mpya: Magufuli Balaa – Kala Pina