Waziri Mkuu Mstaafu ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa amejibu madai ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Abdallah Bulembo kuwa aliwahi kumsaidia shilingi milioni 40 za kampeni.
Bulembo ambaye pia ni Mbunge wa kuteuliwa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jana aliliambia gazeti la Mwananchi kuwa aliwahi kuiomba kambi ya Lowassa kiasi cha shilingi milioni 40 ili zimsaidie katika kampeni za uchaguzi wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, mwaka 2014, kiasi ambacho anadai alipewa na kambi hiyo.
“Unajua kipindi kile nagombea uenyekiti nilimfuata Lowassa nikaomba anichangie katika kampeni zangu, naye alinipa shilingi milioni 40,” Bulembo anakaririwa.
Alidai kuwa kambi hiyo iliutumia msaada huo kama fimbo wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais, baada ya kuona kuwa hamuungi mkono Lowassa kwani alikuwa akimuunga mkono Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda. Alisisitiza kuwa hakuwahi kuwa kambi ya Lowassa na kwamba baada ya kuona wanamzonga kwa kumuita msaliti, aliahidi kuuza gari zake mbili ili awarudishie kiasi hicho cha fedha alichopewa kama msaada. Lakini hakufanya hivyo.
Hata hivyo, Lowassa alikanusha vikali madai hayo ya Bulembo akiyaita upuuzi usio na ukweli wowote.
“Sio kweli,” alisema Lowassa. “Huo ni upuuzi, upuuzi mtupu,” alisisitiza katika mahojiano yake na gazeti hilo kuhusu madai ya Bulembo.
Katika hatua nyingine, Bulembo alikiri kuwa kuondoka kwa Lowassa ndani ya CCM kulizua mpasuko mkubwa katika kipindi cha uchaguzi, na kwamba kwa mara ya kwanza Wajumbe wa Halmashauri Kuu walisimama na kuimba wana imani na ‘Lowassa’ mbele ya Mwenyekiti wa chama hicho, Dkt. Jakaya Kikwete.
Bulembo alidai kuwa endapo Lowassa asingeingia Chadema na kupewa nafasi ya kugombea urais, leo hakuna ambaye angekuwa anamzungumzia na jina lake lingefutika kwenye vichwa vya watu.
Mwanasiasa huyo ambaye tayari ameshatangaza kutogombea tena nafasi ya Uenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi alimshauri Lowassa kupumzika na kuachana na siasa kwani hatakuja kufanikiwa kuwa rais.