Edward Lowassa, ambaye ni mgombea urais kupitia Chadema na mbunge wa jimbo la Monduli anayemaliza muda wake, amemsihi mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Namelock Sokoine kujiunga na Chadema ili awe katika chombo salama.

Akiwahutubia maelfu wa wananchi wa jimbo hilo alilolitumikia kwa kipindi cha miaka 20 kama Mbunge, Lowassa alitumia muda kumsihi mgombea huyo wa CCM kuachana na chama hicho na kumfuata alipoelekea kwa kuwa basi alilopanda (CCM) ni bovu.

“Nimekuwa mbunge wa miaka 20, hivyo natakiwa nimjue mbunge anayefuata. Nitakubaliana na Namelock, akikataa kupanda kwenye basi hili basi,” alisema Lowassa.

Namelock anatajwa kuwa moja kati ya watu waliokuwa karibu na Lowassa wakati akiwa katika Chama Cha Mapinduzi.

Naye waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, alitumia dakika kadhaa kumsihi Namelock kurudisha kadi ya CCM ili ajiunge na timu ya Chadema aliyoiita timu ya Mabadiliko kwa kuwa wakati wa kufanya hivyo ni sasa.

“Namelock ni mtoto wetu tumemsaidia, tumemtunza lakini hatuwezi kumsaidia kwa kuwa amebaki kwenye gari bovu,” alisema Sumaye.

Hata hivyo, Edward Lowassa alihitimisha mjadala huo kwa kumtambulisha rasmi mgombea wa Chadema, Julius Kalanga na kumtaja kuwa ndiye anayepaswa kuwa mrithi wake.

Lowassa alitumia nafasi hiyo pia kuwaomba kura wananchi wa eneo hilo na kuwataka wamsaidie kumuombea kura kwa ndugu na rafiki zao wengine.

 

 

 

Kingunge Aitosa Rasmi CCM Na Kujiunga Na 'Mabadiliko', Hotuba Yote Hapa
Blatter Awagomea Wadhamini Wakuu Wa Fifa, ‘Sijiuzulu’