Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema akiungwa mkono na vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa, Edward Lowassa ametoa ushauri kuhusu njia bora zaidi itakayopelekea kupatikana kwa muafaka utakaomaliza mkwamo wa kisiasa visiwani Zanzibar, uliotokana na kufutwa kwa uchaguzi.

Lowassa ameeleza kuwa ni vyema zaidi kuhakikisha maridhiano hayo yanahusisha watu ambao hawahusiki katika mzozo huo tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo viongozi wa CCM na CUF ndio pekee wanaozungumza.

“Naona wangeshirikisha watu zaidi ya hao ili muafaka upatikane. Hili jambo limechukua muda mrefu sana,” alisema Lowassa.

Katika hatua nyingine, Lowassa alilaani vitendo vinavyoashiria ubaguzi vilivyoonekana katika baadhi ya mabango yaliyobebwa na vijana wa CCM katika sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar zilizofanyika visiwani humo, Januari 12.

“Ni kauli ambayo inaweza kutuletea madhara katika nchi. Ni kauli ambayo baba wa Taifa aliwahi kutuonya tusibaguane. Tusiweze kubaguana kwa rangi, kwa sura, kabila au kwa chochote kile kitakachoharibu nchi yetu,” Lowassa anakaririwa.

Kadhalika, Mwanasiasa huyo mkongwe jana alitembelewa na uongozi wa timu ya wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo wanaojulikana kama Timu Mabadiliko waliofika ofisini kwake jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumpongeza kwa busara zake katika kuimarisha amani na utulivu nchini kabla na baada ya uchaguzi mkuu.

Lowassa akiwa katika picha ya pamoja na wafanyabiashara wa Kariakoo

Lowassa akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa wafanyabiashara wa Kariakoo wa Timu Mabadiliko

 

Andy Carroll Aendelea Kukumbwa Na Majanga
Vumbi La Ligi Kuu 2015-16 Kuendelea Kutimka Wikiendi Hii