Mgombea urais kupitia Chadema, Edward Lowassa ameelezea mikakati ya vipaumbele 12 ambavyo ataanza navyo ndani ya siku 100 endapo atachaguliwa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akiongea jana katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam, Lowassa alisema kuwa katika siku 100, serikali yake itashughulikia masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na suala la kuweka mfumo rafiki wa kodi kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa na kuondoa mfumo wa EFD.

Alieleza pia kuwa atahakikisha anaboresha huduma za afya, hususan huduma za uzazi pamoja na kuunda tume maalum ya kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji.

“Katika siku 100 za serikali yangu, nitanitahakikisha mambo yafuatayo; madawa na vifaa vya uzazi kwa kina mama wote kwenye hospitali zote za serikali vitajazwa. Nitapunguza foleni ya Dar es Salaam. nitaondoa kero kwa wafanya biashara. Kodi kwa mfumo wa EFD nitaiondoa, serikali itakuja na mfumo bora wa kodi na rafiki kwa wafanyakazi wadogo na wakubwa.  

“Nitafuta ada na michango yote ya shule kuanzia Kindergaten hadi chuo kikuu. Nitatengeneza mkakati wa kuondoa tatizo la maji nchini. Nitakuja na mkakati kabambe wa michezo na sanaa. “Nitaunda tume ya kutatua matatizo ya migogoro ya wafanyakazi na wakulima. Nitaanzisha kituo kipya kila wilaya cha kushughulika na matatizo ya wafanyakazi. Watu wakiwa na shida na huduma ya serikali kunakuwa na one center. Hutakiwi kuambiwa nenda jengo hili… nenda jengo lile, ili kupunguza urasimu na rushwa.

“Nitapunguza kodi ya mishahara kwa wafanyakazi, wafanyakazi wanalipa kodi kubwa sana, tutapunguza. Nitaboresha maslahi ya polisi na wanajeshi. Hawa wanatulinda lakini mambo yao makubwa mabovu, wako hoi bin taaban. Tutaunda jeshi dogo na la kisasa na linalipwa mishahara inayostahili.

“Ndugu zangu, mambo haya 11 ndio nitakayoangalia kwenye serikali yangu. Kama nikijaliwa, itakuwa serikali ya speed kali sana ya maendeleo, speed 120 kwa saa.”

 

 

Jaji Lubuva Achoshwa Na Chadema, Awataka Wazibe Madirisha…
Tanzania Yapanda Viwango Vya Soka Duniani