Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amezungumzia namna ambavyo yeye na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wanavyosubiri kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Lowassa amewataka wanachama wa Chadema kuhakikisha kuwa wanakuwa wamoja katika kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu wa 2020. Alisema kuwa anaamini katika chaguzi zilizopita ‘walifung goli’ lakini halikukubaliwa.
“Napenda kuwaomba tujipange vizuri kwa ajili ya uchaguzi wa 2019 na 2020. Tuwe wamoja, tukiwa wamoja tutawashinda vyama vingine, tukianza maneno ya chinichini na tusipokuwa wamoja itakuwa sio vizuri. Tutashinda tukienda kwa umoja wetu na kuacha maneno ya kugombana kila mahali na kila saa,” Mwananchi wanamkariri Lowassa.
Katika hatua nyingine, mwanasiasa huyo alizungumzia hoja inayotumiwa na baadhi ya wadau nchini kuwa amekuwa akisifia utendaji kazi wa Serikali ya Rais John Magufuli.
“Nataka niliweke vizuri hili, kwamba sisi tungepewa nafasi tungefanya vizuri zaidi. Wale wanaonihukumu kuwa ninampa [Rais Magufuli] bila sababu. Sifa zangu ziko qualified kwamba kama amefanya vizuri ingekuwa sisi wapinzani tungefanya vizuri zaidi,” alieleza.
Alisitiza kuwa anaamini uchaguzi ujao utakuwa na nafasi kwa vyama vya upinzani kwani Serikali ya CCM imefanya mambo mengi mazuri na kuleta matatizo mengi pia.
“Nadhani mambo ni mazuri. Kwa sababu mambo ambayo Serikali ya Magufuli inafanya tangu iiingie madarakani ni makubwa na yenye matatizo makubwa,” alisema Lowassa.
Aidha, Lowassa alisema kuwa anasali sana ili mikutano ya hadhara iruhusiwe na kwamba endapo itaruhusiwa atakuwa wa kwanza kuzunguka mikoani kwa lengo la kuwashukuru wapiga kura zaidi ya milioni sita waliomuunga mkono.