Mbio za uchaguzi mkuu zinaendelea kushika kasi kuelekea Oktoba 25 ambapo wananchi wataamua nani aingie ikulu huku kila mgombea akivuta pumzi ya kuhakikisha anakimbia zaidi ya wenzake.

Mgombea urais wa Chadema kupitia Ukawa, Edward Lowassa, amewataka wananchi kuhakikisha kuwa wanakiondoa madarakani chama cha mapinduzi mwaka huu na kwamba wasipoweza mwaka huu hawataweza tena.

Mgombea huyo ambaye ameonesha kuvuta pumzi ya mwisho kisiasa kuweka nguvu zaidi ya kucheza karata yake ya kuiongoza serikali ya awamu ya tano, ameyasema hayo wakati akiwahutubia wananchi katika viwanja vya Gangilonga, Iringa Mjini.

Lowassa aliwaambia wananchi hao kuwa anahitaji kupata kura milioni 10 mwaka huu ili apate asilimia 90 ya kura zitakazopigwa kumuwezesha kuingia ikulu. “Nataka kura nyingi ili hata wakiiba tushinde, asilimia 90 ziwe zenu, hizo 10 waache waibe,” alisema.

Aidha, aliwatia moyo wafuasi wa Ukawa kwa kutaja majina ya vyama vikubwa vya siasa barani Afrika vilivyoondolowa madarakani na vyama vya upinzani kuonesha kuwa hiyo inawezekana pia Tanzania.

“Msipoiondoa CCM mwaka huu hatutaiondoa tena, CCM na Tanu walikuwa na marafiki zao lakini karibu wote wameondoka. Chama cha KANU Kenya kimeshaondoka madarakani, Malawi (Congress Party) nacho kimeondoka, UNIP cha Zambia na kile chama cha Dk. Milton Obote cha Uganda kimeondoka, na tunaona jinsi ambavyo rais wa Zimbabwe anavyohangaika,” alisema.

Lowassa alivitaja tena vipaumbele vya Chadema endapo wataingia madarakani huku akiahidi kuwaletea wananchi maendeleo kwa kasi.

Edward Lowassa na Duni Haji wasindikizwa na wananchi Iringa

Edward Lowassa na Duni Haji wakisindikizwa na wananchi, Iringa

Lowassa na timu yake ya Ukawa walipokelewa vizuri na kukamilisha kazi yao ya Kampeni huku umati mkubwa wa wananchi ukiwaunga mkono na kulisukuma gari la mgombea huyo na mgombea ubunge wa jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa kwa kilometa kadhaa.

Magufuli: Tanzania Haihitaji Vyama Vya Siasa
Picha: Mama yake Zari afika Nyumbani kwa Diamond kumuona ‘Tiffah’