Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amewapa ujumbe baadhi ya makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao majina yao yaliondolewa katika orodha ya wagombea wa nafasi za ndani ya chama hicho kwa kigezo cha kuwa ‘Timu Lowassa’.

Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema amewataka makada hao kumfuata aliko katika kambi ya upinzani kwa madai kuwa anafurahia uhuru wa kifikra na demokrasia ndani ya chama chake.

“Nimesoma na kusikia baadhi ya waliokuwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi majina yao yamekatwa ama kutetea nafasi zao au kugombea kwa sababu mbalimbali, na jina langu limekuwa likitajwatajwa humo,” amesema Lowassa kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari.

“Mimi nawaambia hawa Watanzania wenzetu waliokatwa huko CCM, nawakaribisha huku Ukawa wafurahie demokrasia. Huku niliko kuna maisha mazuri ya kisiasa, Uhuru wa fikra na demokrasia halisi,” aliongeza.

Mwanasiasa huyo nguli aliongeza kuwa Mwalimu Nyerere alileta mfumo wa vyama vingi vya siasa ili kuwapa Watanzania uwanja mpana zaidi wa kufanya siasa.

Magazeti yaTanzania leo Oktoba 6, 2017

“Kwa wote waliokatwa na wanahisi wameonewa waondokane na unyonge wa fikra kudhani kuwa bila CCM hakuna maisha. Waje huku tafanye siasa kwa manufaa ya wananchi wetu,” Lowassa aliandika.

Lowassa alihama CCM mwaka 2015 baada ya jina lake kukatwa kwenye kinyang’anyiro cha wagombea urais. Alihamia Chadema na kupewa nafasi ya kugombea nafasi hiyo akiungwa mkono na vyama vya upinzani vilivyounda ngome ya Ukawa.

Meya wa Jiji la Dar kutegua kitendawili cha mafuriko
Video: Familia ya Lissu yamjibu IGP Sirro, Kiama raia wa kigeni