Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa jana aliwasihi wafuasi wa chama hicho kuendelea kuwa watulivu na kutofanya fujo muda mfupi baada ya Jeshi la Polisi kuzuia mkutano wake wa ndani wilayani Mbarali mkoani Mbeya.

Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu wa Zamani alijikuta akishindwa kuingia kwenye ukumbi uliopangwa kufanyika mkutano wa ndani wa chama hicho, baada ya askari wa Jeshi la Polisi wakiongozwa na Mkuu wa Polisi wilaya ya Mbarali, L. Muhaji kufunga ukumbi huo na kumzuia yeye na viongozi wengine wa chama kuingia ndani huku mamia ya wafuasi wa chama hicho wakionekana maeneo hayo.

Mwanasiasa huyo mkongwe alifanya juhudi ya kuzungumza na Mkuu huyo wa Polisi wa wilaya hiyo huku akijaribu pia kumtafuta Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla lakini juhudi zote hazikuzaa matunda.

Kufuatia hatua hiyo, alitoa wito kwa wanachama wa Chadema kuwa watulivu huku akiwapa pole kwa usumbufu.

“Wananchi endeleeni kuwa watulivu, polisi wamezuia mkutano halali lakini msifanye fujo yoyote. Pokeeni maelekezo kwa viongozi kwa sababu nitarudi tena siku nyingine, poleni sana kwa adha mliyoipata.

Aidha, alililaumu Jeshi la Polisi kwa madai kuwa limekuwa likitumiwa vibaya na watawala kwa kufanya mambo kinyume cha sheria na taratibu.

Alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeamua kuvunja demokrasia na kuvunja sheria namba 5 ya vyama vya siasa ya mwaka 1992.

Mrema ataka Chadema wasibembelezwe
Maneno Ya Mwambusi Baada Kipigo Cha 3-1 Dhidi Ya TP Mazembe