Sauti na kauli za mgombea urais wa Chadema anayewakilisha ngome ya Ukawa, Edward Lowassa imeonekana kuwa adimu kwenye vyombo vya habari katika kipindi cha saa 32 hadi habari hii inapoenda hewani, hali inayochukuliwa kama mkakati thabiti wa kujinoa kwa pambano.

Lowassa ambaye wiki kadhaa zilizopita amekuwa akiteka vichwa vya habari huku takwimu zisizo rasmi zinaonesha kuwa jina lake limesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza mauzo ya magazeti, amekuwa kimya ghafla ndani ya muda tajwa hapo juu huku wapinzani wake (CCM) wakisikika zaidi wakimrushia vijembe na kumdhihaki.

Katika muda huo, CCM wameteka vichwa vya habari hasa baada ya kutangaza Kamati yenye makada 32 wakiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana kwa lengo la kupambana na Lowassa. Wakimnadi mgombea wa chama hicho, Dk. John Magufuli.

Kauli mbalimbali za viongozi wa CCM wa ngazi ya Taifa katika kipindi hiki zimejikita haswa katika kumshambulia Lowassa.

“Namjua sana Lowassa, huyu jamaa hafai… hafai hata kuwa balozi wa nyumba kumi,” alisema Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye japo chama hicho hicho ndicho kilichomteua kuwa Waziri Mkuu wa serikali ya awamu ya nne inayomaliza muda wake.

Mwenyekiti wa CCM, Dk. Jakaya Kikwete jana alionesha wasiwasi wake kuwa picha za mafuriko ya Lowassa hutengenezwa kwa kompyuta ili kuonesha umati mkubwa zaidi ya watu tofauti na uhalisia. Huku akiwaambia wanachama wa chama hicho kuwa picha halisi zitaonekana wakati wa kampeni za chama hicho.

Hata hivyo, Lowassa ameendelea kuwa kimya baada ya kumaliza ziara yake ya kutafuta wadhamini na hata alipofuatwa na waandishi wa habari jana wakati alipomaliza kusaini fomu ya kiapo katika Mahakama Kuu, alisema ataongea muda ukifika.

Ni dhahiri kwamba Lowassa na kambi ya Ukawa  wameamua kujipa mapumziko ya kuzungumza ikiwa ni mkakati wa kuisoma vyema safu ya wapinzani wao na kutafuta majibu ya kauli zao huku wakisubiri kipenga cha NEC kuanza mbio za kampeni mapema kesho kutwa (Agosti 22).

Ingawa watanzania wameshafahamu kuwa CCM itafanya uzinduzi wa kampeni katika viwanja vya Zakhem Mbagala jijini Dar es Salaam, Ukawa bado hawajaeleza sehemu watakayofanyia uzinduzi wao hasa baada ya ombi lao la kutumia uwanja wa Taifa kukataliwa na serikali.

Uchaguzi wa mwaka huu unaweka historia katika nchi hii kutokana na nguvu kubwa zinazoonekana katika pande zote mbili. Chochote kinaweza kutokea na yeyote anaweza kuwa rais wa Tanzania hasa kati ya Edward Lowassa na Dk. John Magufuli.

UVCCM Yatoa Onyo Chadema Kutumia Red Brigade
Figisu Figisu Za Usajili Ulaya