Hatimaye waziri mkuu aliyejiuzulu na mbunge wa Monduli, Edward Lowassa leo amechukua fomu za kugombea urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Tukio hilo lililofanyika katika makao makuu ya chama hicho yaliyoko Kinondoni, Dar es Salaam limeshuhudiwa na mamia ya wananchi wanaomuunga mkono katika harakati zake za kuwania kuingia ikulu.

Lowassa aliungwa mkono na mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ambaye hakuwepo wakati anatambulishwa rasmi na kupewa kadi ya chama hicho, hali iliyozua tetesi kuwa hakubaliani kabisa na uamuzi uliofanywa na viongozi wenzake na kwamba aliamua kujiondoa katika chama hicho.

Akiongea na waandishi wa habari katika tukio hilo, Tundu Lissu alianza kwa kukanusha taarifa hizo akidai kuwa zilikuwa porojo za mitandaoni huku akiwataka wananchi kuzipuuza.

Lissu aliongeza kuwa uamuzi wa kumchagua Lowassa kuwa mgombea wa kiti cha urais kupitia Chadema na baadae Ukawa haukufanywa kwa kukurupuka.

“Tumefanya utafiti aina ya Wagombea ambao tunawahitaji, mpaka kumpata Lowassa kazi kubwa imefanyika,” alisema. “’Viongozi wa Chama walishirikishwa kumpitisha Lowassa kugombea Urais, haukuwa uamuzi rahisi na haukuwa wa kushtukiza,” aliongeza Tundu Lissu.

Aliongeza kuwa mkakati wa Chadema ni kuhakikisha ngome yao inashinda viti 133 vya ubunge ili waziri mkuu achaguliwe kutoka chama hicho endapo watashinda katika uchaguzi wa urais mwezi Oktoba.

Akizungumzia tuhuma zilizokuwa zikielekezwa na chama hicho kwa Lowassa, Lissu alisema kuwa wamegundua kuwa hana tatizo na kwamba hajawahi kukwepa kodi ya serikali hivyo ana sifa zote za kugombea urais kupitia chama hicho.

Naye Edward Lowassa alipopewa nafasi ya kuzungumza machache huku akichukua tahadhari kuwa huenda maneno yake yakatafsiriwa kuwa ni kuanza kampeni mapema, Lowassa alisema kuwa wanaomshambulia wanapoteza muda na hawatamyumbisha.

fomu 2

“’Kazi nitakayoifanya ndiyo itakuwa shukrani yangu, najiandaa kufanya kazi iliyotukuka. Umaskini upo Tanzania tangu mwaka 1962 hakuna mabadiliko, wapeni watu wengine wafanye kazi,” Lowassa anakaririwa.

Mgombea huyo anatarajia kuanza kuzunguka baadhi ya mikoa ya Tanzania kwa ajili ya kutafuta udhamini na ridhaa ya wanachama wa Chadema kabla ya mchakato rasmi wa kuanza kampeni akiwakilisha ngome ya Ukawa.

 

Maradona Atangaza Vita Na Vimelea Vya Rushwa
Rio de Janeiro Ina Kasoro, Michezo Ya Olympic 2016