Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa amebeza juhudi za kampeni za CCM katika jimbo la Monduli pamoja na jiji la Arusha kwa ujumla akidai kuwa eneo hilo ni eneo linalohitaji mabadiliko.

Akiongea na wananchi jijini Arusha katika eneo la Ngaramtoni, Jimbo la Arumeru Magharibi, Lowassa alisema kuwa CCM itapata majibu yake Oktoba 25 kwa kuwa wananchi wataiondoa madarakani.

“Nimeona CCM wakipitapita Monduli na Arusha, nawaambia wasubiri tarehe 25 Oktoba huu ndio mwaka wao wa kutoka madarakani. Siku ikifika nendeni vituoni na vichinjio vyenu mkawakate,” alisema Lowassa.

Aidha, Lowassa aliuambia umati wa wananchi waliofurika kumsikiliza huku wakishangilia kwa kumuita ‘rais, rais, rais’ kuwa wahakikishe wanampigia kura za kutosha na wakeshe vituoni kuzilinda kwa kuwa kumuita rais pekee hakuwezi kumpeleka Ikulu.

Lowassa aliwaahidi pia wananchi hao kuwa atahakikisha anaondoa kero ya maji kama alivyofanya katika jimbo lake la Monduli alilolitumikia kama mbunge kwa miaka 20.

Aliongeza kuwa wakati anatatua kero za maji katika jimbo la Monduli kwa kuwapelekea maji, aliwapa viongozi wa Arumeru bure pampu mbili za maji ili kuwasaidia katika kuwaletea wananchi hao maji lakini hazikuzaa matunda.

“Kulikuwa na pampu nne, mbili zikapeleka maji Monduli, mbili nikawapa viongozi wa Arumeru ili wawaletee maji, tena niliwapa bure hizo pampu, sasa mimi ningefanya nini zaidi ya hapo?” Alihoji.

Lowassa aliwambia wananchi hao kuwa pindi atakapoingia madarakani atahakikisha anapambana na umasikini, kutoa elimu bure na bora kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu pamoja na kuwezesha kilimo cha kisasa.

“Watakulima wataruhusiwa kuuza mazao popoe na hawatakuwa na ushuru wowote kwenye mazo yao,” alisema.

Leo, Lowassa anatarajiwa kufanya mkutano mkubwa jijini Arusha unaotarajiwa kuanza majira ya mchana. Arusha inatajwa kuwa ngome ya Chadema.

 

Kimenuka Kambi Ya Super Eangles
Mzee Kingunge Kupanda Jukwaa La Ukawa Jijini Arusha, Leo