Mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye leo watapanda jukwaa moja la siasa ikiwa ni mara ya kwanza tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu, Oktoba 25.

Lowassa na Sumaye wataungana na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wengine wa Ukawa kurusha kete zao katika kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema katika mkutano wa hadhara utakaofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Sinoni.

Mwenyekiti wa Chadema wa Arusha Mjini, Dereck Magoma amesema kuwa ametoa taarifa kwa jeshi la polisi kwa ajili ya kuhakikisha ulinzi kwa kuwa wanatarajia kuwa na umati mkubwa wa wananchi.

Magoma aliwaambia waandishi wa habari kuwa tayari wabunge wote wa Kaskazini wameshafika Arusha kwa ajili ya kumnadi Lema ambapo watapiga kambi hadi uchaguzi huo utakapofanyika Disemba 13 mwaka huu kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Uchaguzi huo uliahirishwa baada ya kutokea kifo cha aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Arusha Mjini kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Estomiah Mallah.

Magufuli atinga Feri, awapa wavuvi namba yake ya simu, awaahidi mambo matatu
Kamati Kuu CCM Yamkata Manji