Wakati joto la uchaguzi likiongezeka kila siku, Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa amewataka watanzania kuvumilia matatizo wanayoyapata kwa kuwa baada ya siku 60 hali itabadilika.

Lowassa ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na makundi mbalimbali ya wajasiriamali jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku moja kabla ya siku ya kufanya uzinduzi wa kampeni za ngome ya Ukawa (leo), katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam.

Wawakilishi wa makundi hayo walimueleza matatizo mbalimbali wanayokutana nayo katika shughuli zao na kumuomba ayatatue atakapopata ridhaa ya kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Hao wanaowafanyia hivyo waache waendelee tu ila baada ya siku 60 yatakwisha. Hatuwezi kuongeza nchi wakati watu wengine hawanufaiki, na tofauti kati ya tajiri na masikini inazidi kuwa kubwa na serikali haisahihishi hilo, haiwezekani,” Lowassa alisema.

Mgombea huyo wa Chadema aliendelea kusisitiza kuhusu adhama yake ya kulikomboa taifa kutoka katika umasikini.

“Haiwezekani watu wengine wabaki masikini wakikosa haki yao katika taifa lao, haiwezekani. Nasema Mungu akijalia nikawa rais nitabadilisha kwa kasi inayostahili na nguvu inayostahili, nawaahidi,” aliendelea.

Leo, Ukawa watazindua rasmi kampeni zao katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam huku maelfu ya wananchi yakitarajiwa kuhudhuria.

CCM Wamnyemelea Lowassa Dakika Za Mwisho
Mwakyembe Amng’ang’ania Lowassa Kashfa Ya Richmond