Kocha Mkuu wa Young Africans Luc Eymael ameeleza kushangazwa na mamlaka za usimamizi wa soka nchini (TFF), kuruhusu matumizi ya uwanja wa Karume unaotumiwa na Biashara United.
Akizungumza baada ya timu yake kulazimishwa sare tasa dhidi ya Biashara United jana Jumapili mjini Musoma, Mara, Eymael alisema uwanja huo hauna hadhi ya kutumika kwa ajili ya mpira wa miguu.
“Ni aibu kwa timu kubwa kama Yanga kucheza katika uwanja huu ambao hadhi yake ni ya kuchungia mifugo, vyumba vya kabadilisha nguo havifai, inashangaza kuona wasimamizi wa mpira wanaruhusu uwanja huu kuendelea kutumika,” alisema Eymael.
“Mimi nawafundisha wachezaji wangu kucheza kandanda safi la burudani, lakini haiwezekani kucheza katika kiwanja kama hiki. Nawapongeza wachezaji wangu wamepambana, tumekosa bahati tu.”
Aidha Eymael amesema matokeo hayo yamemvurugia mipango yake lakini wataendelea kupambana mpaka mwisho kuhakikisha wanatimiza malengo ya kumaliza katika nafasi ya pili.
Azam FC iliipiku Young Africans kwenye nafasi ya pili baada ya kuifumua Singida United mabao saba kwa sifuri. Young Africans itacheza na Singida United baada ya mchezo wao wa Kombe La Shirikisho Tanzani Bara (ASFC) dhidi ya Simba SC.