KOCHA wa Mabingwa wa Kihistoria nchini (Young Africans), Luc Eymael amesema anahitaji wachezaji saba tu katika usajili wa dirisha kubwa ili kuboresha kikosi chake kwa ajili ya ushiriki wa Ligi na michuano mengine ambayo klabu itashiriki.
Kocha huyo ambaye bado nchini kwao Ubelgiji, amesema naamini usajili wa wachezaji saba anaowahitaji utakua chachu ya maboresho ya kikosi chake kwa msimu ujao, ambapo amedhamiria kurejeshea heshima ya ubingwa wa Young Africans.
Amesema tayari ameshawasilisha ripoti kwa viongozi, na anachosubiri ni utekelezaji wakati wa dirisha la usajili litakapofunguliwa rasmi.
“Nimewasilisha repoti ambayo ina mahitaji kwa nafasi husika, huwezi kubomoa kikosi kwa kiwango kikubwa, timu ni nzuri na inahitaji maboresho kidogo tu hivyo nikipata wachezaji saba bila shaka nitakuwa na kikosi imara sana msimu ujao,” anasema kocha.
Amesema kwa sasa bado hawezi kuzungumzia mchakato wa usajili kwa kuwa dirisha la usajili bado lakini kama kocha kuna watu amewaona hapa Tanzania na wengine nje ya nchi ambao anadhani wanafaa kuja kuongeza nguvu.
“Kwa sasa hatuzungumzii usajili, tunazungumzia mapendekezo tu, kwa hiyo nimewasilisha kwa uongozi na ninaamini wao watafuatilia kwa kila mchezaji kwa mujibu wa taratibu za usajili ili kuona nani tunaweza kumpata na nani hatuwezi na mbadala wake atakuwa nani,” anasema.
Luc kwa sasa yuko nchini Ubelgiji baada ya kusimama kwa Ligi kutokana na janga la ugonjwa wa Corona na ameacha repoti yenye mapendekezo yakuongeza wachezaji saba kwenye kikosi.