Meneja wa klabu ya Inter Milan Luciano Spalletti ameelezea uwezekano wa kufanya kazi na kiungo na nahodha timu ya taifa ya Croatia Luka Modric, ambaye yu tayari kuondoka kwa mabingwa wa soka barani Ulaya Real Madrid, katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi.
Spalleti amezungumzia uwezekano huo, baada ya kusaini mkataba mpya na klabu ya Inter Milan ambao utamuwezesha kukinoa kikosi cha klabu hiyo hadi mwaka 2021.
Akizungumza mara baada ya shughuli ya kusaini mkataba huo, meneja huyo kutoka nchini Italia alisema ni mapema mno kuzungumzia uhakika wa ujio wa Modric, lakini kuna uwezekano wa kufanya kazi na mchezaji huyo msimu ujao.
Alisema mipango ya kusajiliwa kwake inaendelea kufanywa na viongozi wa ngazi za juu, na amekua akisisitiza jambo hilo lifanywe kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili, lakini bado akasisitiza uhakika wa kutua kwa Modric mjini Milan utategemea na mazungumzo yanayoendelea baina ya viongozi wa pande hizo mbili, licha ya kuwepo kwa uwezekano wa kuwa pamoja siku za usoni.
“Nipo tayari kufanya kazi na mchezaji huyu, uwezekano huo upo, japo sina uhakika sana.”
“Ninaamini viongozi wangu watakamilisha taratibu za mazungumzo na kuushawishi uongozi wa Real Madrid ili tuweze kumpata kwa msimu ujao na miaka mingine, kwa sababu ninavutiwa sana na uchezaji wake.” Alisema Spalletti kumwambia mwandishi wa Sky Sport Italia.
Mwishoni mwa juma lililopita viongozi wa Inter Milan walitarajiwa kukutana na Rais wa Real Madrid Florentono Perez kwa ajili ya mazungumzo ya uhamisho wa Modric, na inasemekana huenda pande hizo mbili zikakubaliana kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa majira ya kiangazi mwishoni mwa mwezi huu.