Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ameliagiza jeshi la polisi mkoani Arusha kumkamata haraka Mkurugenzi wa Kampuni ya Ortello Business Corporation (OBC) kwa tuhuma za kuajiri raia wa kigeni bila kufuata sheria.
Lugola ambaye anaendelea na ziara yake katika wilaya sita za mkoa huo, juzi aliwaambia waandishi wa habari kuwa mkurugenzi huyo anayefahamika kwa jina la Isack Mollel alitakiwa kujisalimisha polisi tangu wiki iliyopita lakini hakufanya hivyo.
Kwa mujibu wa Waziri Lugola, kuna takribani wafanyakazi kumi wa kampuni ya OBC ambao wanafanya kazi bila kuwa na kibali.
Amesema kuna baadhi ya raia hao wa kigeni wamefunguliwa kesi mahakamani kwa kosa la kuingia nchini kinyume cha sheria na kesi yao itatajwa Februari 22 mwaka huu.
Hata hivyo, Waziri hakutaja nchi watokazo raia hao wa kigeni pamoja na kazi ambazo wamekuwa wakifanya kwenye kampuni hiyo.
Kwa mujibu wa sheria, raia wote wa kigeni wanaofanya kazi nchini wanapaswa kuwa na kibali maalum kinachowatambua kulingana na kazi husika wanayoifanya.