Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesema kuwa kuna baadhi ya polisi wasiokuwa waaminifu nchini wanaoshirikiana na mafisadi kudhulumu ardhi ya wananchi maskini, sasa dawa yao imeiva.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Haruzale, Kata ya Nyamihyolo, Jimbo la Mwibara, Bunda mkoani Mara akiwa katika ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo jimboni mwake, ambapo amesema kuwa amepokea malalamiko mengi ya ardhi katika jimbo lake na sehemu mbalimbali nchini.

Amesema kuwa mafisadi wa ardhi hukimbilia kufungua kesi vituoni wakilazimisha kwa kutumia fedha ardhi iwe mali yao wakiwatumia polisi wasiokuwa waaminifu ili kufanikisha matwaka yao.

“Haiwezekani tabia hii ikachekewachekewa na kuonekana ni kawaida, nimekemea sana katika mikutano yangu hapa Mwibara na sehemu zinginezo hapa nchini, nitahakikisha napambana na mafisadi pamoja na polisi hao wasiokuwa waaminifu,” amesema Lugola.

Aidha, Lugola amesema kuwa kila kukicha anapata malalamiko mengi kutoka sehemu mbalimbali nchini kuwa mafisadi wanaendelea kuwaonea wananchi maskini kwa kupora ardhi wakidai wao ndio wamiliki halali.

Hata hivyo, amewataka wananchi wa Mwibara kuhifadhi vyakula vyao vizuri ili kuepusha janga la njaa kwa hapo baadaye na kusababisha wananchi kuja kuteseka kwa ukosefu wa vyakula na kusababisha mateso katika familia.

 

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 7, 2019
Magogo ya kukatia Nyama buchani yapigwa marufuku