Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amefanya ziara ya kushtukiza katika Kituo cha Polisi Stakishari kilichopo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufuatilia utendaji kazi wa Kituo hicho.
Lugola amekutana na wananchi mapokezi ya kituo hicho ambao walifika kwa ajili ya kuwachukulia dhamana ndugu zao waliopo katika mahabusu ya kituo hicho, aliwahoji kama wanapata huduma nzuri kutoka kwa askari wa kituo hicho.
Pia Waziri Lugola akiwa katika mapokezi ya kituo hicho, alikichukua kitabu cha taarifa za watuhumiwa wote waliopo mahabusu na baadaye kuelekea katika mahabusu hiyo akiwahoji watuhumiwa wote kwa kuwaita kwa majina kujua makosa yao yaliyoyafanya wawepo kituoni hapo.
Akizungumza mara baada ya kumaliza kuwahoji mahabusu hao, amesema kuwa ziara yake ni ya kawaida ya kufuatilia utendaji kazi wa vituo vya polisi, pia kufuatilia ahadi zake ambazo alizitoa Bungeni kufuatilia vituo mbalimbali vinavyolalamikiwa, na pia yeye Waziri ni wajibu wake kufuatilia utendaji kazi pamoja na maagizo anayoyatoa mara kwa mara ya dhamana zitolewe saa 24 ikiwemo Jumamosi na Jumapili na pamoja na polisi kutowabambikizia kesi wananchi.
“Lengo la hii ziara yangu ni kuboresha utendaji kazi wa vituo vya polisi nchini, sijaja kumuadhibu mtu mimi, hivyo msiwe na wasiwasi, bali kilichonifanya hapa nije nikufuatilia maagizo mbalimbali ambayo niliyatoa kama kweli mnayafanyia kazi,” amesema Lugola.
Hata hivyo, Lugola amewataka Makamanda wa polisi mikoa mbalimbali nchini, kusimamia utendaji kazi bora na kuhakikisha maagizo yake anayoyatoa yanafanyiwa kazi ipasavyo, na ataendelea kuyafuatilia maagizo yote anayoyatoa na endapo yakipuuzwa hatamvumilia mtu.