Familia iliyokuwa imeususa mwili wa ndugu yao uliokuwa umehifadhiwa mochwari, Salum Kindamba imeamua kukubali na kuuzika mwili huo jana mara baada ya kushauriana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola.

Familia hiyo iliususa mwili huo mochwari ya Hospitali ya Taifa Muhimbili tangu Agosti 11 huku ikisisitiza kutozika hadi itakapopata majibu ya kilichosababisha ndugu yao auawe akiwa mikononi mwa polisi.

Awali, familia hiyo ililishutumu jeshi la polisi kwa kumpiga risasi ndugu yao na kusababisha kifo chake.

Lakini, msemaji wa familia amesema juzi walifika ofisini kwa waziri huyo na kushauriana, kisha akawaomba wasitishe mgomo huo kwa vile alikuwa katika hatua za mwisho kupata ufumbuzi wa suala lao.

Mwili wa Salum uliachwa mochwari kwa muda wa siku 19 huku familia ikisisitiza kuendelea na mgomo huo hata kama ungekaa  mwaka mmoja.

Aidha mwili wa marehemu ulizikwa katika makaburi ya Karakata, Kipawa.

Kwa mujibu wa msemaji wa familia, Waziri Lugola ameahidi kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo siku chache zijazo na atafanya hivyo baada ya kupokea ripoti kutoka katika timu yake inayofuatilia suala hilo.

Familia imetoa shukrani za dhati kwa Waziri Lugola kwa ushirikiano mkubwa alioutoa na kuahidi kushughulikia suala hilo na tayari ameanza kushughulikia.

Kwa wa taarifa zilizotolewa na Jeshi la Polisi marehemu Salum Kindamba aliuawa kwa kupigwa risasi ya mguuni na kiunoni na polisi mara baada ya yeye na wenzake watatu kushikiliwa huku yeye akijaribu kuwakimbia polisi na mfuko uliokuwa ukitiliwa mashaka na jeshi la pilisi uliokuwa na bastola aina ya pistol, pesa pamoja na simu aina ya Tekno.

 

 

Lucas Moura kurudisha heshima Tottenham Hotspurs
Mwamunyange ateuliwa na Rais wa Zimbabwe