Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ameagiza kukamatwa kwa dereva wa basi lililotaka kusababisha ajali ambayo yeye angekuwa mhanga, katika eneo la Gairo mkoani Morogoro.
Imeripotiwa kuwa basi hilo la ‘Hekima za Mungu’ lenye namba za usajili T140 AZZ lililokuwa likisafiri jana mchana kutoka Dar es Salaam kuelekea Kahama liliipita gari iliyokuwa mbele yake (overtake) katika kona kali isiyoruhusiwa kufanya hivyo, huku mbele yake akielekea kukutana uso kwa uso na gari lililombeba Waziri Lugola aliyekuwa akitoka jijini Dodoma kuelekea jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Waziri Lugola, dereva wake aliyekuwa katika upande sahihi alilazimika kupunguza mwendo ili kuepuka ajali.
Kufuatia kitendo hicho, Waziri Lugola aliagiza vyombo vya dola kulizuia gari hilo ambapo alifika na kuzungumza na abiria huku akiwashangaa kwa kutochukua hatua za kumkanya dereva huyo.
“Kwanini mnashindwa kukemea hii tabia ya huyu dereva, mnataka awaue? Aliwahoji abiria. “Alitaka kusababisha ajali mbaya sana hapa. Nanyi mmekaa kimya. Mnafanya makosa kutoripoti hii tabia mbaya kabisa,” Waziri Lugola anakaririwa.
Ingawa dereva wa basi hilo, Issack Vian alikiri kufanya kosa na kuomba msamaha, Waziri Lugola aliagiza akamatwe punde atakapowafikisha abiria mjini Kahama.