Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amewataka viongozi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyopo chini ya Wizara yake nchini, kuacha tabia ya kuwanyanyasa askari waliochini yao na wahakikishe wanawapandisha vyeo, wanarekebisha mishahara, pamoja na kulipwa fedha za likizo.
Amesema kuwa kuna idadi kubwa ya askari wanaostahili kupandishwa vyeo na kurekibishiwa mishahara, kwa kuwa askari hao wana haki kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Askari na Watumishi wa Wizara yake, mjini Ifakara, Wilaya Kilombero, Mkoani Morogoro, Lugola amesema kuwa katika uongozi wake hataki kusikia askari wananyanyaswa na kiongozi yeyote wa Taasisi zake.
Amesema kuwa unyanyasaji, kutokupandisha vyeo, pamoja na kulipwa fedha zao za likizo, changamoto hizo zinapunguza nguvu ya utendaji kazi wa askari hao wanaofanya kazi ngumu.
“Kwanini bado hamjapanda vyeo na kubadilishiwa mishahara yenu mpaka sasa wakati nilishatoa maelekezo mpandishwe, nitahakikisha nalifuatilia hili mapema zaidi ili nijue tatizo ni nini, lakini naamini kila kitu kinaenda vizuri na ahadi niliyoitoa itakamilisha kwa wale askari ambao wanasifa watapewa vyeo hivi karibuni,”amesema Lugola.
Pia Lugola amezungumzia kuhusu ukosefu wa nyumba za makazi ya askari, kuwa licha ya Rais Dkt. John Magufuli kutoa mchango mkubwa kwa kulisaidia Jeshi, lakini bado kuna upungufu mkubwa wa nyumba hizo.
Aidha, Lugola amesema kuwa changamoto nyingine inayowakabili askari wa vyombo vyake ni kutopata fedha za kuhamishwa na atahakikisha madai yote ya askari hao yanafanyiwa kazi.
Waziri Lugola yupo Mkoani Morogoro kikazi na tayari amemaliza ziara yake Wilaya ya Kilombero, na anatarajia kufanya ziara hiyo katika Wilaya za Malinyi na Ulanga Mkoani humo.