Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewataka wananchi kuwahurumia askari wa jeshi la polisi na kuwasaidia kama wanavyofanya kwa watumishi wa sekta nyingine.
Akizungumza kwenye mkutano uliowahusisha wananchi na polisi, Waziri Lugola alihoji kuhusu tabia njema ya wananchi kuchangia katika sekta za elimu na afya lakini wamekuwa wakiitenga sekta ya ulinzi na usalama ambayo ni muhimu.
“Tunachanga kujenga zahanati, tunachanga kuwajengea walimu nyumba, tunachanga kumjengea afisa tarafa nyumba. Lakini naomba anyanyuke hapa Mtanzania yeyote hapa Saunga aniambie ni lini amechanga kujenga kituo cha polisi na ni lini amechanga kujenga nyumba za polisi,” amesema Lugola.
Akifafanua changamoto za makazi pamoja na kazi za askari wa jeshi hilo, Lugola ameeleza kuwa jeshi hilo lenye askari takribani 45,800 lina asilimia 20 pekee ya nyumba za makazi.
Alisema askari hao wamekuwa wakifanya kazi muda wote bila kujali siku ya mapumziko, sikukuu au hali ya hewa, hivyo aliwaomba wananchi kuwaonea huruma.
“Tuhakikishe kama tunahitaji kuwa na usalama na jeshi la polisi la kutulindia mali zetu na sisi tumelala tunasherehekea, ili hali wao wanafanya kazi, ni lazima tuwe na huruma na askari hawa na tuone umuhimu wa kusaidia jeshi la polisi,” alisema.
Tangu alipoteuliwa kuwa Waziri, Lugola aliahidi pamoja na mambo mengine kuhakikisha maisha ya askari wa jeshi la polisi pamoja na mazingira yao ya kazi yanaboreshwa.