Waziri ya mambo ya ndani ya nchi Kangi Lugola amewatahadharisha Watanzania wanaoendelea kushiriki biashara ya kusafirisha au kuwahifadhi wahamiaji haramu kuwa wataozea jela badala ya kufurahia maisha ya uraiani.
Lugola ameyasema hayo Jijini Dodoma hii leo Novemba 15, 2019 muda mfupi baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuwajengea uwezo maofisa wa uhamiaji baina Serikali na Shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia wahamiaji (IOM).
Amesema hakuna mtu yeyote atakayevumiliwa na Serikali kwa kujihusisha na biashara hiyo na kwamba ni wajibu wa kila mtanzania kufuata taratibu na sheria za nchi ili kuendeleza utulivu na amani iloyopo bila kujihusisha na mambo yasiyofaa ikiwemo uhalifu.
“Kupanga ni kuchagu sasa kama utachagua jela we endelea kushiriki biashara ya kuficha au kusafirisha wahamiaji haramu lazima utaozea jela na hutofaidi matunda ya uhuru yaloyopo uraiani hivyo niwatahadharishe wale wote wenye tabia kama hii kuiacha mara moja,” amebainisha Waziri Lugola.
Majaliwa aitahadharisha jamii madhara ya ulaji usiofaa
Kuhusu mafunzo hayo amesema yatatolewa katika Chuo cha Uhamiaji cha Kanda kilichopo Moshi Mkoani Kilimanjaro ambacho kimekuwa kikitoa taaluma ya uhamiaji kwa maofisa uhamiaji wa Tanzania na nje ya nchi huku mkataba huo ukiwa umesainiwa baada ya ule wa awali wa miaka mitano kumalizika.
Aidha amesema katika kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama kwa kudhibiti matukio ya uhalifu nchini, Serikali imekubaliana na Shirika hilo kupitia Wizara ya mambo ya ndani kupata mafunzo, teknolojia na baadhi ya vifaa ili kukabiliana na matukio ya wahamiaji haramu.
“Suala la uhamiaji haramu linatakiwa kukomeshwa na ili kuhakikisha tunapambana nalo tumeona ni vyema tukakubaliana na shilika la IOM ili kupata mafunzo na teknolojia ikiwemo na vifaa kwa minajili ya kudhibiti vitendo vya uhamiaji haramu,” amefafanua Waziri wa mambo ya ndani Kangi Lugola.
Kwa upande wake Mwakilishi mkazi wa IOM Dkt. Qasim Sufi amesema shirika hilo limeamua kusaini mkataba na nchi ya Tanzania baada ya ule wa awali kuisha kwa manufaa kwani ulitekelezwa baada ya kutoa mafunzo kwa maofisa wa uhamiaji ambao walikabiliana vyema na wahamiaji haramu.
“Suala la kupambana na wahamiaji haramu si la nchi moja kwani linahitaji ushirikiano wa kutosha hivyo kila nchi barani Afrika inatakiwa kuhakikisha inaungana juhudi za mapambano kuhakikisha tatizo hili linapungua na hatimaye kufikia malengo,” amesisitiza Sufi.
Naye Kamishna wa Uhamiaji ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha uhamiaji cha Kanda kilichopo Mkoani Kilimanjaro Maurice Kitunusa amesema shirika hilo limekuwa likiwajengea uwezo wa kujiendesha wenyewe kwa kuandaa wataalamu wenye uwezo wa kutoa ushahidi mahakamani kuhusu taarifa mbalimbali.