Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema kuwa atafuatilia kwa kushtukiza utekelezaji wa agizo la Serikali kuhusu pikipiki za kubeba abiria maarufu kama bodaboda zinazoshikiliwa katika vituo vya polisi.
Lugola amesema kuwa atahakikisha agizo hilo linatekelezwa na atawachukulia hatua watakaolipuuzia.
Waziri Lugola aliwaagiza polisi wakati akizungumza bungeni kuhakikisha hawazishikilii bodaboda ambazo zina makosa madogo kama ya kofia ngumu au kubeba abiria zaidi ya mmoja.
Alisema kuwa pikipiki ambazo zitakuwa zinashikiliwa polisi ni zile ambazo zimekamatwa kwa kushiriki katika uhalifu na zile zilizokosa wamiliki.
“Hawatajua siku, saa wala muda, watashtukia tu nimeibukia kwenye kituo chao. Nataka suala hili liishe ili niondoe malalamiko ya vijana kuhusu bodaboda zao,” Lugola anakaririwa na Mwananchi, jana.
Aliongeza kuwa endapo atakuta kuna pikipiki zinazoshikiliwa kituoni hapo kinyume na maagizo ya Serikali, itatimia ile kauli aliyoisema bungeni ya ‘ama zangu ama zao’.