Mfanyabiashara Said Lugumi (kulia -pichani) ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Lugumi Enterprises, amesema kuwa watendaji kupitia Jeshi la Polisi ndio waliomkwamisha kutekeleza kikamilifu mkataba wa kufunga vifaa vya utambuzi wa alama za vidole.
Mwaka 2001, Kampuni hiyo ya Lugumi ilipewa mkataba wa kufunga vifaa vya utambuzi wa alama za vidole katika vituo 108 vya polisi, lakini hadi mwaka huu kampuni hiyo pamoja na kulipwa asilimia 99 ya malipo ya Sh34 bilioni ilikuwa imefunga katika vituo 32 tu.
Kampuni hiyo kupitia kwa mwanasheria wake, Onesmo Mpinzile imesema kuwa walikwamishwa kwa kutowekewa mazingira ya kukamilisha mkataba wao kama ilivyoainishwa kwenye mkataba husika.
“Kama alivyosema [Waziri] Lugola, mteja wangu anataka kumaliza swala hilo lakini upande mwingine wanamkwamisha,” Mwananchi wanamkariri Mpinzile.
“Polisi au Serikali wanamkwamisha mteja wetu ambaye kutokana na suala hili kufikia hatua mbalimbali anataka kumaliza suala hili na kufikia muafaka,” aliongeza.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola hivi karibuni alisema kuwa baada ya kufanya mazungumzo na Lugumi pamoja na viongozi wa jeshi la polisi walibaini kuwa kuna mambo ambayo jeshi hilo halikutekeleza yaliyokwamisha utekelezaji wa mkataba.
Alisema kuwa pamoja na mambo mengine, Lugumi alimueleza kuwa baadhi ya maeneo ambayo alipaswa kufunga mashine hizo bado hazijaunganishwa na mkongo wa taifa na kwamba kuna baadhi ya vituo hakukuwa na mahala pa kufunga mashine hizo.
“Unachokisikia ukiwa nje, ukiingia ndani ni mambo mengine. Hapo ni sisi [Serikali] kupitia jeshi la polisi tulitakiwa kukamilisha baadhi ya mambo ili yeye aweze kufunga,” Waziri Lugola alisema kwenye kipindi cha ‘Tunatekeleza’ cha TBC1.
Aliongeza kuwa kutokana na hali halisi, aliomba apewe muda wa miezi minne ili aweze kutekeleza baada ya hali hiyo kuwekwa sawa na kwamba walikubaliana hivyo.
Sakata la Lugumi ni moja kati ya masakata yaliyolitikisa Bunge baada ya kubainishwa kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya Mwaka wa Fedha 2013/14.
Ripoti hiyo ilibainisha kuwa ni vituo 14 tu vilikuwa vimefungwa mashine hizo wakati kampuni ya Lugumi ikiwa imeshalipwa asilimia 99 ya malipo ya Sh34 bilioni.