Aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Hispania Luis Enrique amesisitiza hana mpango wa kuchukuwa nafasi ya Kuliongoza Benchi la Ufundi la Klabu ya Tottenham Hostpurs, baada ya kuondoka kwa Antonio Conte mwishoni mwa juma lililopita.
Kocha huyo amekuwa akihusishwa na klabu ya Tottenham Hotspur, sambamba na Kocha wao wa zamani Muaricio Pochettino na Kocha wa Frankfurt, Oliver Glasner na Julian Nagelsmann ambaye alifungashiwa virago FC Bayern Munich.
Taarifa za kutimuliwa kwa Antonio Conte zilithibishwa baada ya sare ya mabao 3-3 dhidi ya Southampton kwenye mechi ya Ligi Kuu England.
Licha ya Enrique kuipotezea Spurs, kocha huyo amedai angependa kufanya kazi katika Klabu za Soka za England siku za usoni lakini sio kwa sasa.
“Napenda kwenda timu ambayo ina uwezo wa kufanya mambo makubwa, hata hivyo sio jambo rahisi kila jambo linahitaji muda, nilipata ofa nyingi kutoka timu za taifa lakini sio klabu, lakini kama ikitokea timu nzuri labda, ila sidhani kama nipo tayari kwa sasa,” amesema Enrique,
Enrique alianza kutengeneza jina lake kuanzia ngazi ya klabu, alicheza soka kulipwa katika timu za Celta Vigo na AS Roma, kabla ya kurejea FC Barcelona ambako alikipiga kwa muda wa miaka minane.
Baada ya kujikita kwenye ukocha, Enrique alikiongoza kikosi cha FC Barcelona na kubeba ubingwa Mataji matatu msimu wa 2014-2015. Enrique aliinoa timu ya taifa ya Hispania katika jumla ya michezo 44 kabla ya kujiengua kikosini baada ya kutolewa Raundi ya 16 Bora ya Fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka 2022.