Mabingwa wa Soka nchini Ufaransa, Paris Saint-Germain wanakaribia kumteua Luis Enrique kuwa kocha mpya wa klabu hiyo kwa ajili ya kuuanza msimu mpya wa 2023-24.
PSG bado haijathibitisha kuachana na kocha wake wa sasa, Christophe Galtier, lakini inaaminika kuwa muda wake katika klabu hiyo utafikia kikomo majira haya ya joto.
Galtier, 56, alitua PSG kuchukua mikoba ya Mauricio Pochettino Julai 2022 lakini alishindwa kufikia matarajio.
Luis Enrique amekuwa akihusishwa na klabu nyingi tangu aachane na timu ya Taifa ya Hispania baada ya Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka jana.
PSG ilimgeukia kocha huyo mwenye umri wa miaka 53 baada ya mazungumzo na meneja wa zamani wa Bayern Munich Julian Nagelsmann kumalizika bila kufikia muafaka.
PSG wana nia ya kuirejesha klabu na kujaribu kujenga timu badala ya kuendeleza sera ya kusajili mastaa lukuki na ghali kwa kuwa hadi sasa mfumo huo umeshindwa kuwapa matunda kwenye Ligi ya Mabingwa.