Kocha wa Mabingwa wa Soka nchini Ufaransa Paris Saint-Germain ‘PSG’, Luis Enrique amesema anapaswa kulaumiwa yeye kwa kichapo kizito cha mabao 4-1 walichokipata kutoka kwa Newcastle United kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyochezwa juzi Jumatano (Oktoba 04).
PSG walizidiwa nguvu na vijana wa Eddie Howe kwenye dimba la St James’ Park, huku Kylian Mbappe na wachezaji wenzake wakijikuta hawana la kufanya.
Shinikizo tayari linaongezeka kwa Kocha huyo raia wa Hispania baada ya kushinda mechi tatu pekee kati ya saba za kwanza za Ligue 1 tangu kuteuliwa kwake msimu huu wa joto na kipigo hicho kitazua maswali zaidi.
Alipoulizwa kuhusu kichapo hicho, Enrique alisema: “Ndiyo, kabisa. Ninapaswa kulaumiwa mimi. Hakuna shaka kuhusu hilo.
“Mimi ndiye mtu wa kwanza kuwajibika kwa hilo. Ninawajibika.
“Matokeo ya mchezo yalikuwa ya haki. Nadhani wachezaji wangu walitatizika kidogo na mchezo. Walifanya kila kitu nilichowaomba wafanye.
“Kwa utu na mtazamo, niliona ni nzuri lakini bila shaka tulifanya makosa ya kizembe ambayo yalisababisha mabao yao.
“Unapocheza kwa kiwango hiki huwezi kufanya hivyo.”
PSG sasa inawafuata Newcastle katika nafasi ya pili katika kundi lao la Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini Enrique hakuona haja ya kuwa na hofu, akipendekeza ukali wa matokeo ulikuwa kwa upande wake.