Hatimae bosi wa kikosi cha FC Barcelona Luis Enrique amethibitisha ataondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu huu, baada ya kutoa huduma ya ukufunzi kwa miaka mitatu.
Enrique aliwaambia waandishi wa habari, hatokuwa sehemu ya benchi la ufundi la FC Barcelona kuanzia msimu ujao kutokana na kuhitaji kupumzika.
Enrique amekua katika shughuli za ukufunzi wa soka huko Camp Nou tangu mwaka 2014, baada ya kuondoka kwa Tata Martino.
Katika utawala wake, Enrique ametwaa ubingwa wa ligi ya Hispania mara mbili, kombe la Mfalme mara mbili na ligi ya mabingwa barani Ulaya mara moja.
Msimu wake wa kwanza alionyesha kuwa safu ya ushambuliaji yenye hatari zaidi, kutokana na muunganiko wa wachezaji watatu kutoka Amerika ya kusini Lionel Messi, Luis Suarez na Neymar.
“Sina budi kuushukuru uongozi wa FC Barcelona kwa imani kubwa walionionyesha tangu siku ya kwanza nilipoanza kazi, daima nitaendelea kuyakumbuka mafanikio niliyoyapata katika miaka mitatu ya ukufunzi wangu,”
“Wakati wa maandalizi ya msimu huu, nilizungumza na wakurugenzi wa Barca, Albert Soler na Robert Fernandez, niliwaambia mwishoni mwa msimu huu, nitapenda kupumzika, hivyo sina uhakika kama nitasaini mkataba mpya.
“Waliniambia hakuna haraka ya kufanya maamuzi hayo, lakini umefika wakati nimeona hakuna namna, zaidi ya kutimiza hadai niliyoiweka tangu mwezi July mwaka jana.” Alisema Enrique.