Imefahamika kuwa Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Msumbuji na Klabu ya Al Ahly ya Misri, Luis Miquissone, ametua nchini kimya kimya na kupokewa na mabosi wa Simba SC kwa ajili ya kuendelea na mazungumzo ya kumsajili kwa ajili ya msimu mpya.

Simba SC imekuwa ikihaha kumrudisha nyota huyo ambaye ilimuuza kwa mabingwa wa Afrika, Al Ahly mwaka juzi lakini hakufanikiwa kupata namba katika kikosi cha kwanza cha Waarabu hao.

Hali hiyo ilisababisha Al Ahly kumtoa kwa mkopo katika klabu ya Abha ya Saudi Arabia, ambayo tayari amemaliza mkopo huo na kurejea kwenye timu yake ‘mama’.

Taarifa zilizopatikana kutoka Simba SC zinasema jina la Miquissone limepitishwa katika orodha ya wachezaji wanaowindwa lakini ikimhitaji kwa usajili wa mkopo ambao wanaitaka AlAhly kusaidia kumlipa mshahara nyota huyo.

“Miquissone yupo tayari nchini na amefikia katika kambi ya Simba SC, na hayupo peke yake, wapo wachezaji wengine ambao hawajaenda Uturuki kutokana na uongozi kushughulikia changamoto zao ili kukamilisha taratibu za safari. Wakati wowote wanaweza kumtangaza kama mchezaji mpya wa Simba SC.

Unajua hakuna kitu ambacho kinawapa wakati mgumu uongozi kama lawama wanazopata kutoka kwa mashabiki, ndio maana wamekuwa makini sana”, kimesema chanzo chetu cha habari hii.

Alipotafutwa Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema kwa sasa bado hawajatambulisha wachezaji watatu.

“Nadhani hatujamaliza, wapo ambao tutaendelea kuwatambulisha na kuna mchezaji mmoja mkubwa sana ambaye utambulisho wake nchi itaenda kutikisika,” amesema Ahmed.

Ameongeza uongozi wa klabu hiyo umeahidi kuendelea kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa ambao utawapa matokeo chanya na furaha katika msimu mpya.

Karate Tanzania kushiriki Maziwa makuu
Simba SC kufunguwa African Football League