Kiungo Mshambuliaji wa zamani wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Jose Luis Miquissone, amesema bado anaamini wababe hao wa Msimbazi wana nafasi ya kutetea taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2021/22.

Miquissone anayeitumikia Al Ahly ya Misri, ametoa kauli hiyo alipohojiwa na Mtandao wa Goal.com, kutoa mtazamo wake kuhusu Simba SC ya msimu huu ambayo imeonesha kuwa na mapungufu na kuiacha Young Africans ikitamba kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu.

Kiungo huyo kutoka nchini Msumbiji amesema hana shaka na uwezo wa Simba SC, na kilichotokea ni sehemu ya mchezo wa soka, hivyo ni mapema mno kwake kukubali kama klabu hiyo imepoteza heshima ya ubingwa wa Tanzania Bara.

Amesema mbali na Ligi Kuu Tanzania Bara, pia anaiona Simba SC ikiwa katika nafasi nzuri ya kufikia malengo kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.

“Bado naipa nafasi kubwa timu yangu (Simba) kufanya hivyo lakini hata katika mashindano mengine kama kombe la Shirikisho (ASFC), nalo wanaweza kufanya vizuri na kuchukua ubingwa.” amesema Luis Miquissone

Kiungo huyo aliyesajiliwa Msimbazi akitokea UD Songo ya nchini kwao Msumbiji mwanzoni mwa mwaka 2020, amekua na wakati mgumu wa kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha Al Ahly tangu alipotua jijini Cairo mwanzoni mwa msimu huu.

Ashindwa kuondoka Ukraine baada ya kubadili Jinsia
Dullah Mbabe, Shehe Haji watambiana