Kiungo kutoka nchini Croatia na klabu ya Real Madrid Luka Modric ametangaza hadharani kutaka kuona Mshambuliaji wa PSG Kylian Mbappe akijiunga na The Galacticos msimu ujao 2022/23.
Modric ametoa kauli hiyo saa chache baada ya Real Madrid kuibamiza PSG kwenye mchezo wa hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya jana Jumatano (Machi 09).
Mkataba wa Mbappe unamalizika mwishoni mwa Juni na fowadi huyo wa Paris Saint-Germain anaendelea kuhusishwa na kutaka kuhamia Madrid.
Modric pia anakaribia mwisho wa mkataba wake, lakini amezungumzia nia yake ya kuongeza muda wake wa kukaa na vinara hao wa LaLiga Madrid, na mshindi huyo wa Ballon d’Or 2018 amesema mchezaji yeyote duniani angemtaka Mbappe awe mchezaji mwenzake.
“Tunataka kucheza na wachezaji wakubwa, Kylian ni mmoja wa hao. Bila shaka, ningependa kucheza naye, tuone,” kiungo huyo aliwaambia waandishi wa habari.
“Ni vigumu kuzungumzia wachezaji wengine, klabu zinakasirika, vinaweza kutafsiri vibaya, lakini sidhani kama kuna mchezaji asiyemtaka kwenye timu yao.” amesema Modric
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23 alijumuishwa kwenye kikosi cha PSG kilichominyana na Real Madrid jana Jumatano (Machi 09) katika mchezo wa mkondo wa pili wa hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mbappe ndiye aliyekuwa tofauti katika mchezo wa kwanza, akifunga bao la ushindi dakika za lala salama na kuwapa PSG faida ya 1-0 baada ya Lionel Messi penati yake kuokolewa na kipa wa Madrid, Thibaut Courtois.
Mbappe amehusika moja kwa moja katika mabao 18 katika michezo 13 ilizopita kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, akifunga mabao 13 na kusaidia mengine matano.
Bao lake la ushindi katika mchezo wa kwanza lilikuwa bao lake la mwisho kabisa katika mashindano hayo hadi sasa, akifunga baada ya dakika 93 na sekunde 14.
Sehemu kubwa ya azimio la PSG kumbakisha Mbappe licha ya ofa kutoka kwa Madrid mwaka jana ilikuwa nia yao ya kushinda Ligi ya Mabingwa.