Mchezaji wa Manchester United, Romelu Lukaku huenda akakitosa kikosi cha Wekundu hao wa Old Trafford kutokana na kuvurugwa kiakili na Jose Mourinho, tangu Oktoba mwaka huu.
Tetesi za mshambuliaji huyo kutoka nchini Ubelgiji kuachana na timu hiyo ya Uingereza, zimefanana na sababu ambazo zinatajwa pia kwa sakata la Paul Pogba na Alexis Sanchez.
Hata hivyo, mkataba wa Lukaku unakuwa kisiki kisichoweza kung’oka kirahisi mwezi Januari kama ulivyo mtazamo wa mashabiki wengi wa soka duniani.
Fukuto hilo la kupoteza morali kwa wachezaji muhimu wa timu hiyo ambao wamekuwa wakirusha lawama zao kwa Mourinho linakorezwa na kufanya vibaya kwa timu hiyo msimu huu, ikihitaji miujiza kuwa kati ya timu nne zilizo nafasi ya juu kwenye ligi hiyo inayoongozwa na Manchester City. Wekundu hao wa Old Trafford wako nyuma kwa alama 18 dhidi ya Man City kwenye Ligi Kuu ya Uingereza.
Hata hivyo, wakati Mourinho akitajwa kuwa miongoni mwa makocha ambao wanaweza kukumbwa na panga la kutumbuliwa msimu huu, wakala wake Jorge Mendes amesema kuwa Mourinho anayafurahia maisha ndani ya Man United akila bata na kwamba hata uongozi wake pia unafurahishwa na kazi anayoifanya.
“Kumekuwa na tetesi kuwa Mourinho anaondoka Man United, sio kweli. Ana furaha ndani ya klabu na anafurahia maisha. Ana mkataba wa muda mrefu na Man United na amejitolea kikamilifu katika kuijenga timu inayoleta ushindi,” alisema Mendes.
Lukaku amehusika katika kikosi kinachoanza kwenye michezo miwili pekee tangu mwezi Oktoba, na alirudishwa benchi na Mourinho katika mchezo dhidi ya Arsenal. Hali hiyo inatajwa kumchanganya kiakili kama ilivyo kwa Sanchez na Pogba.
Sanchez ameenda nchini kwao Chile kwa ajili ya kupata matibabu ya kurejesha hali ya kiakili (rehab) pamoja na majeraha.