Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amelitaka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kulipa kodi ya ardhi katika eneo inalolimiliki la Viwanda lililopo Weruweru wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro kabla ya desemba mwaka huu.
Amewataka wote waliokuwa katika eneo hilo bila ya hati wala offer kutoendelea kuwepo eneo hilo kwa kuwa hawana uhalali wa kumiliki maeneo katika eneo la Weruweru.
Amesema kuwa ufanyike ukaguzi kwa kila kiwanja katika eneo la viwanda la Weruweru lenye ukubwa wa ekari 1103 kwa lengo la kubaini viwanja vyote visivyoendelezwa na watakaobainika watanyang’anywa maeneo hayo kwa mujibu wa sheria.
NDC inamiliki eneo la viwanda lenye ukubwa wa ekari 626 kikiwemo kiwanda cha kutengeneza mashine mbalimbali kama vile za kusaga, kukoboa na kuranda mbao cha Kilimanjaro Machine Tools Manufacturing Co Ltd ambapo kati ya ekari hizo 80 tayari zina hati huku ekari 546 zikiwa na offer.
Aidha, Lukuvi ameshangazwa na NDC kushindwa kulipa kodi ya ardhi katika kipindi chote wanachomiliki eneo hilo huku wakiwakodisha wananchi kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo na kueleza kuwa Shirika hilo la Maendeleo la Taifa litakapo lipa kodi yote ya ardhi litapatiwa hati ya umiliki katika eneo lenye offer.
“Kosa lenu NDC mnakodisha watu masikini halafu ninyi hamlipi kodi ya ardhi sasa mnatakiwa kulipa kodi ya ardhi tangu mlipoanza kumilikishwa eneo hilo kufikia desemba mwaka huu 2018” amesema Lukuvi
Kwa mujibu wa waziri Lukuvi katika eneo hilo la viwanda la Weruweru kuna watu wameshikilia maeneo kwa muda mrefu tangu mwaka 1985 bila kuyaendeleza huku wengine wakibadilisha matumizi hivyo ameagiza wote wapewe Ilani ya ubatilisho na ikibidi serikali itafuta miliki zao na kuyagawa maeneo hayo kwa watu wengine ili wajenge viwanda.
-
Serikali yamkaanga Wema Sepetu
-
JPM aitaka wizara ya kilimo ijitathmini
-
Lugumi aeleza alivyokwamishwa kufunga mashine polisi
Hata hivyo, Meneja wa kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools Manufacturing Co Ltd, Andreano Nyaluke alijitetea kwa kusema kushindwa kulipa kodi ya ardhi katika muda wote wa umiliki kunatokana na uwezo mdogo wa kiwanda ingawa amesema jitihada zinafanyika ikiwemo kutafuta mkopo kwa ajili ya kuendeleza kiwanda.