Aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amemkabidhi Ofisi aliyekuwa Naibu wake Dkt Angeline Mabula ambaye sasa ni Waziri wa Wizara hiyo.
Makabidhiano ya ofisi yamefanyika leo Februari 17 2022 kwenye ofisi za Wizara hiyo katika mji wa serikali Mtumba jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Lukuvi amesema ana furaha kubwa kumkabidhi ofisi mtu anayeijua Wizara na aliyekuwa akifanya kazi naye.
‘’ Dkt Angela anayajua mengi kwenye wizara, tumeshirikiana katika kushughulukia dhuluma na malalamiko ya ardhi na katika kipindi chote tumejitahidi kupunguza malalamiko na yamepungua’’. Amesema Lukuvi.
‘’Ninaomba mumpe ushirikiano, nimefanya naye kazi takriban miaka sita na tumeelewana sana na nilimpa kazi nyingi kwa sababu ana uwezo, tofauti yangu mimi na yeye ni kuwa, mimi ni mkali ila yeye ni mpole’’ Amesema Lukuvi.
Aidha ameishukuru Menejiment ya Wizara kwa kuonesha ushirikiano wakati wa kipindi chote alichokuwa Wizara ya Ardhi na kuitaka menejiment hiyo kumpa ushirikiano Waziri wa sasa Dkt Mabula.
Kwa upande wake Dkt Mabula mbali na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan pia kwa kumuamini na kumteua kuwa Waziri wa Ardhi, huku akimshukuru Lukuvi kwa kumpa uhuru wa kufanya kazi wakati wote alipokuwa wakifanya kazi pamoja.
Waziri Dkt Mabula aliongeza kuwa, pamoja na mambo mengine lakini msisitizo wa wizara yake kwa sasa mbali na mambo mengine ni vipaumbele vya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika masuala ya uwekezaji na mifumo ya utunzaji kumbukumbu za ardhi.
Aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye ni Mbunge wa jimbo la Isimani mkoani Iringa William Lukuvi aliondolewa nafasi ya uwaziri katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika mapema januari mwaka huu. Lukuvi aliteuliwa kwa mara ya kwanza nafasi ya uwaziri mwaka 1995 katika iliyokuwa wizara ya kazi na baadaye kuhudumu Ofisi ya Waziri Mkuu na baadaye Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambako alidumu kwa miaka 8 tangu mwaka 2014.