Serikali imetoa Siku 30 kufuatia kusimamishwa kwa maofisa ardhi 183 wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kufanyika uchunguzi kwa watendaji hao waliowafutia wateja madeni ikiwemo kupunguza saizi ya ukubwa wa viwanja kupitia mfumo wa malipo na kuisababishia serikali hasara ya mapato yatokanayo na viwanja.

Baada ya uchunguzi huo wale watakaobainika kutenda makosa hayo hatua Kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao huku wale ambao hawatakutwa na makosa watarejeshwa Kazini.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na  Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ambapo amesema kuwa timu iliyoundwa kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa watendaji waliohujumu mfumo wa ulipaji malipo ya viwanja itawajumuisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na taasisi nyingine ambazo zina wataalamu wanaohusika na mifumo inayotumia mitandao.

Amesema kuwa watendaji waliosimamishwa kazi wamebainika ndani ya miezi sita ya mwaka wa fedha 2018/19 ambapo mfumo wa malipo Hazina ndio umepelekea wao kubainika kwa sababu unaonyesha moja kwa moja.

“Naomba muelewe hawa waliosimamishwa hivi sasa ni wale walioiibia serikali kuanzia shilingi laki moja na kuendelea, lakini katika uchunguzi utakaofanywa hata kama umeiibia serikali shilingi moja utachukuliwa hatua za kisheria,” amesema Lukuvi.

Aidha amewataka waliobaki nao wajiandae na zoezi hilo maana baada ya uchunguzi kuna majina mengine yatabainika kwa sababu wanaanzia kuchunguza tokea mfumo ulipoanza kutumika.

Hata hivyo, Lukuvi ameongeza kuwa walioshirikiana na watendaji wa Wizara hiyo kufanya mchezo huo wasifikiri wako salama bali watalipa kiasi cha fedha ambacho amefutiwa deni ikiwemo kupunguziwa ukubwa wa kiwanja ambacho amekuwa akilipa fedha pungufu.

 

VIDEO: Hatima ya Lissu kurejea kujulikana Agosti 20, Kikwete asimulia siri ya kuanzishwa kwa SADC
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 10, 2019