Serikali imetangaza mkakati mpya wa kupima na kuipanga ardhi yote nchini huku kipaumbele kikiwekwa katika kuwapatia ardhi wawekezaji hasa katika sekta ya viwanda ndani ya siku saba tu na kurasimisha makazi ya kaya maskini.
Magaeuzi hayo yametangazwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alipokuwa akizungumza katika kipindi cha “TUNATEKELEZA” kinachoandaliwa kwa pamoja kati ya TBC1 na Idara ya Habari-MAELEZO.
“Tumeanza kutekeleza mpango wa miaka 10 wa kuhakikisha kila kipande cha ardhi katika nchi hii kinapimwa na kupangiwa matumizi,” alisema akigusia kuwa mradi huo umeanza kutekelezwa mkoani Morogoro na utaendelea nchi nzima.
Kutokana na mpango huo na pia kubadilika kwa utendaji ndani ya wizara yake, Waziri Lukuvi anasema kuwa kuanzia sasa wawekezaji wote nchini ni marufuku kwenda moja kwa moja vijijini kununua ardhi.
“Wapite Kituo cha Uwekezaji na kama pale watakosa ardhi waje wizarani kwangu. Tuna ardhi ya kutosha na tunajua ilipo. Tutawapatia wawekezaji hasa wanaotaka kuwekeza katika viwanda ardhi ndani ya siku saba tena bila rushwa wala urasimu,” alisema.
Katika kuhakikisha kuwa wizara ya Ardhi inakuwa kitovu cha kusaidia utekelezaji wa azma ya Tanzania ya viwanda, Waziri Lukuvi pia amegusia kuwa Serikali imeshatenga maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda.
Alitaja kutengwa kwa takribani viwanja 240 katika Manispaa ya Kigamboni, Dar es Salaam kwa ajili ya viwanda na kwamba wizara yake inaendelea kubaini maeneo mengine nchini ikiwemo kwa kuwanyang’anya ardhi hiyo watu waliojilimbikizia bila kuitumia.
“Zile nyakati za mtu kujilimbikizia ardhi kubwa bila kuitumia zimekwisha. Mheshimiwa Rais ametuagiza na sisi tunafanyiakazi, tumeamua sasa tutaitwaa ardhi hiyo na kuwa wanaotaka kuwekeza,” alisisitiza.
Kuhusu tabia ya baadhi ya watanzania kujilimbikizia viwanja na ardhi, Waziri Lukuvi amesisitiza kuwa anaandaa mwongozo wa kuweka ukomo wa mtu kumiliki ardhi Tanzania. Mkakati huo utakamilika ndani ya mwaka huu.
Akigusia makazi ya watu maskini, alisema Serikali imekwishaanza utekelezaji wa mradi wa kurasimisha makazi yaliyojengwa kiholela ili kuwapa hati wananchi wa maeneo hayo ili ardhi yao iwe na thamani.
“Tumeanza zoezi hili kule Kimara na Chasimba, Dar es Salaam. Wananchi wakiuelewa mradi huu vyema na kutoa ushirikiano watafaidika nao kwani unalenga kuboresha makazi yao, kuwawekea miundombinu muhimu na zaidi kuwapimia maeneo yao ili waweze kuwa na hati,’ alisema.
Waziri Lukuvi pia ametumia muda huo kuwakemea maofisa wa umma wanaosababisha migogoro ya ardhi nchini na kusisitiza kuwa muda wao wa kufanyakazi kwa mazoea na kiujanjaujanja umekwisha.
“Wananchi wengi wamedhulumiwa ardhi tena kwa makosa ya watendaji wetu. Kwa Dar es Salaam tumeanza kuwapa heshima ya kuwafidia wananchi wa aina hiyo kwa kuwapa viwanja vingine zaidi ya 600. Ole wao watendaji watakaoendelea kusababisha migogoro hiyo,” alionya.
Mpango wa Pili wa Miaka Mitano unaazimia kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Maono na nia ya Waziri Lukuvi katika kuleta mageuzi katika wizara yake ni chachu ya mafanikio ya azima ya viwanda

Trump Asisitiza Kujenga Ukuta Kuwazuia Wahamiaji
Mwanadiplomasia Atoa Ushauli Kwa Vyama Vya Siasa,Asema hakuna Haja Ya Maandamano