Mshambuliaji Reliants Lusajo amejiunga na klabu ya KMC FC baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja, akitokea Namungo FC ya mkoani Lindi.

Lusajo amesajiliwa KMC baada ya kumaliza mkataba wake na Namungo FC, ambayo msimu ujao itaiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Akiwa Namungo FC mshambuliaji huyo alionyesha uwezo mkubwa na kuisaidia klabu hiyo kumaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL), na kuwa mshindi wa pili wa Kombe la Shirikisho (ASFC) na kukata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa.

Msimu ulioisha (2019/20), Lusajo alikuwa miongoni mwa wachezaji wazawa waliofanya vyema katika nafasi ya ushambuliaji, akimaliza na mabao 12, huku Yusuf Mhilu akimaliza na 13, kinara akiwa Meddie Kagere wa Simba aliyemaliza na 22.

Meneja wa Lusajo Ahmad Kassim ‘Prezidaa’ alipoulizwa habari za usajili wa mchezaji wake kutimkia KMC FC, alishindwa kukataa ama kukubali, kwani alihimiza subra hadi uongozi wa klabu hiyo utakaposema jambo leo Agosti 19.

“Ujue sina nafasi yakulizungumzia hilo kwa sasa, ila naamini kesho utayapata majibu kamili wakati KMC ikitangaza nyota wake wapya ndani ya kikosi hicho,”amesema.

Wakati huo huo kikosi cha KMC FC jana Jumanne kilianza mazoezi kwenye uwanja wa Bora, Kijitonyama jijini Dar es salaam, huku wachezaji waliosajiliwa katika kindi hiki wakijumuika na wenzao.

Wachezaji waliosajiliwa klabuni hapo ni Martin Kigi, Andrew Vicent, David Mwasa, Masoud Abdallah na Israel Patrick.

Mchezaji mwingine waliofika kwenye mazoezi hiyo jana ni kiungo, Masoud Abdallah ‘Cabaye” ambaye atacheza hapo kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea katika kikosi cha Azam FC.

Kikosi cha KMC FC kimeanza maandalizi hayo kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu chini ya kocha msaidizi, Habib Kondo.

Naibu Waziri amsimamisha kazi Mkurugenzi
‘Diwani’ avuliwa nguo kwenye mkutano baada ya vurugu kuibuka