Mbunge wa Jimbo la Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, kuwahoji Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye, na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana kuhusu sauti zilizovuja ambazo zimedaiwa kuwa na maneno ya fedheha kwa viongozi wa nchi.
Hayo yamesemwa leo Julai 20, 2019, mbele ya wanahabari jijini Dar es Salam huku akiongezea kuwa pamoja na sakata hilo kupamba moto ndani ya CCM amesema hakuna mgogoro isipokuwa kuna watu wachache wanaoulumbana na mtu mmoja mmiliki magazeti nchini, jambo ambalo haliwezi kuitwa mgogoro ndani ya chama hicho.
Hatua hiyo ni kufuatia waraka ulioandikwa na waliokuwa makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Yusufu Makamba kuhusiana na malalamiko yao dhidi ya mmiliki wa magazeti hapa nchini, Cyprian Musiba.
Ambapo kwenye waraka huo Kinana na Makamba wameandika kwa uongozi wa chama kupitia kwa Pius Msekwa, wakisema Musiba amekuwa akiwazushia mambo mbalimbali ya kisiasa bila kuchukuliwa hatua yeyote na mamlaka zilizopo.
”Nataka niseme kuwa wazee wangu wamepotoka kwa kutoa waraka huo; walitakiwa wamtafute kijana wa kumjibu Musiba, au wao wenyewe watafute press (mkutano wa habari) wamjibu Musiba siyo kuandika waraka utakaobaki maishani mwao kwamba viongozi wa kisiasa wa ngazi za juu, Kinana na Makamba, waliuandika kumlalamikia Musiba, vitu ambavyo naona vimewafedhehesha sana.” alisema Lusinde.
Akitetea kauli zake kuhusu kuitwa na kuhojiwa kwa Kinana na Nape, Lusinde amesema:
“Mimi nafurahi Musiba kuwatukana viongozi wastaafu, sababu Kinana alitukana viongozi wake akawaita mizigo, Nape amepata umashuhuri kwa ajili ya matusi, nashangaa wanakasirika nini wakati wameuunda utaratibu huu.”
Akikanusha kwamba ametumwa kuja kutoa kauli hizo, Lusinde amesema amejituma mwenyewe kulisemea jambo hilo.
“Hakuna mbunge anayepangwa, mimi sihitaji kutumwa na mtu, najituma mwenyewe. Mimi sijaja kumtetea Musiba, kazi aliyoifanya Musiba ilikuwa inafanywa na Nape, kwa hiyo wasilalamike hiyo kazi walishaianza wao.
Aidha, amemalizia kwa kusema Kinana na mzee Makamba walikuwa na nafasi ya kuzungumza na Rais John Magufuli na hawakuitumia nafasi hiyo na kuamua kuandika waraka.