Kocha Mkuu wa Azam FC George Lwandamina amelazimika kujipanga kivingine kuelekea mchezo dhidi ya Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC utakaopigwa Jumapili Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.
Lwandamina ambaye atakutana kwa mara ya kwanza dhidi ya Simba SC tangu alipokabidhiwa jukumu la kuwa mkuu wa benchi la ufundi Azam FC, atakua na kazi ya kuhakikisha anapata alama tatu muhimu kwenye mchezo huo ambao Simba SC watakua wenyeji.
Akizungumzia kuhusu maandalizi yao kuelekea mchezo huo, Mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano wa klabu ya Azam FC, Thabith Zakaria ‘Zaka Zakazi’ amesema timu yao inahitaji kujiandaa vyema kuweza kuikabili Simba SC.
“Kikosi chetu kinaendelea na mazoezi kujiandaa na michezo ya mzunguko wa pili wa ligi, tulianza baada ya kukamilika kwa michuano ya Mapinduzi ambapo tumecheza michezo mitatu ya kujipima nguvu.”
“Kati ya michezo hiyo tulishinda michezo miwili, mmoja na kupoteza mchezo mmoja, kabla ya kucheza tena dhidi ya KMC jijini Dar es Salaam, huku tukpata sare ya 1-1 dhidi ya TP Mazembe jana usiku.”
“Michezo hii ni sehemu ya maagizo ya kocha Lwandamina ambaye kwa kutambua ugumu wa mchezo wetu dhidi ya Simba utakaopigwa Februari 07, ameomba kupatiwa michezo mingi ya kujipima nguvu ili kukifanya kikosi chake kiwe tayari kwa mchezo huo.”
“Tunajua Simba wana kikosi kizuri na wameongeza nguvu kupitia usajili lakini hata sisi tumesajili na tumejipanga vizuri.” amesema Zakazakazi
Jana usiku Azam FC walicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya mabingwa wa soka kutoka DR Congo TP Mazembe, na kuambulia sare ya bao moja kwa moja.