Kocha mkuu wa Azam FC George Lwandamina amesema angependa kufanya usajili wa wachezaji katika kipindi cha dirisha dogo la usajilia mbacho rasmi kimefunguliwa leo Jumatano (Desemba 16).

Lwandamina aliyekiongoza kikosi chake kwa mara ya kwanza kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Juzi Jumatatu (Desemba 14) kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi dhidi ya Namungo FC, alisema usajili wa wachezaji klabuni hapo utategemea na kukubaliwa kwa ombi ambalo ataliwasilisha kwa afisa mtendaji mkuu Abdulkarim Amin ‘Popat’.

Alisema endapo atakubaliwa ombi hilo atafanikisha lengo lakuboresha kikosi chake, ambacho kwa zaidi ya mwezi mmoja kimeshindwa kupata matokeo mazuri, kwenye michezo ya nyumbani na ugenini ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Usajili ni kwa ajili ya timu kubwa na sisi pia lazima tufanye usajili kutokana na mapendekezo yangu ambayo nitayatoa nitakapokutana na viongozi kuwaeleza ni wapi na mchezaji gani ambaye atatusaidia kufikia malengo yanayotarajiwa,” alisema Lwandamina.

Alisema upungufu aliouona ni ule ule katika michezo yote miwili dhidi ya Namungo na Gwambina FC ambao alikuwa jukwaani akiishuhudia.

“Timu ni nzuri, lakini kuna upungufu ambao unatakiwa kufanyiwa kazi kipindi cha usajili, nitaweka wazi kwa uongozi kwa kuwaeleza mahitaji na aina gani na nafasi ipi ambayo ninatakiwa kuboresha,” alisema Lwandamina.

Azam FC ambayo imeshuka dimbani mara 15 hadi sasa, ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 28, moja nyuma ya Simba SC iliyopo nafasi ya pili baada ya mechi 13, huku Young Africans iliyocheza mechi sawa na ‘Wanalambalamba’ hao, ikiwa kileleni na alama zake 37.

Kocha Kaze akabidhi jalada kamati ya usajili Young Africans
Mapinduzi CUP 2021: Simba SC, Namungo FC hatarini kushiriki