Kiungo kutoka nchini Uganda na klabu ya Simba SC Thadeo Lwanga amesema yupo tayari kuipigania klabu yake katika Mzunguuko wa Pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao ulianza rasmi mwishoni mwa juma lililopita.

Lwanga ametoa kauli hiyo baada ya kupona jeraha lake, ambalo lilimuweka nje kwa zaidi ya miezi minne, akiumia kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Kiungo huyo ambaye alisafiri na kikosi cha Simba SC katika nchi za Niger na Morocco, amesema anatambua ana jukumu zito sambamba na wachezaji wenzake kuipigania Simba SC katika kipindi hiki, hivyo hana budi kujitoa ili kufikia lengo la kutetea Ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.

“Nilipata majeraha mwezi Oktoba, mwaka jana katika mchezo dhidi Jwaneng Galaxy.”

“Jeraha lilikuwa kubwa, namshukuru Mungu nimepona na nipo tayari kurudi uwanjani na mashabiki watarajie kuniona hivi karibuni hasa kwenye raundi ya pili.” amesema Lwanga

Kurejea kwa Lwanga ndani ya kikosi cha Simba, kunaongeza uimara wa timu hiyo, hasa kwenye safu ya viungo wakabaji ambayo ilikua na wachezaji kama Sadio Kanoute, Muzamiru Yassin na Jonas Mkude.

Kocha Azam FC aivizia Coastal Union
Mwanamitindo wa Ukraine aliyevaa Gwanda kuingia vitani