Kiswahili kimetajwa kuwa ni silaha katika Taifa la Tanzania baada ya kutambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), ikiwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 200 duniani.
Hayo yamebainishwa hii leo Juni 6, 2022 Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa, wakati akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
“Serikali ya Tanzania kupitia Wizara hii inaendelea na mikakati ya kuiongoza dunia kuadhimisha siku hii kwa mara ya kwanza Julai 7, 2022 katika Balozi zetu kote Duniani, kama wasemavyo Waswahili, Hamadi ni ilio kibindoni na silaha ni iliyo mkononi, Kiswahili ndiyo silaha yetu” amefafanua Mchengerwa.
Ameongeza kuwa Lugha adhimu ya Kiswahili imeendelea kukua na kuimarika katika maeneo mbalimbali na kwamba kukubalika kutumika kitaifa, kikanda na kimataifa ni hatua njema inayolitangaza Taifa la Tanzania ulimwenguni.
“Matumizi ya Kiswahili yanazidi kukubalika kitaifa, kikanda na kimataifa na jitihada hizi kwa kipindi cha mwaka 2021/22 zimezaa matunda kwa lugha yetu kuvishwa joho jipya kuwa lugha ya kazi katika Umoja wa Afrika” ameongeza Waziri.
Aidha Mchengerwa ameliambia Bunge kuwa Kiswahili kimepitishwa kuwa lugha ya Kazi ya Umoja wa Afrika katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika Februari 5 – 6, 2022 Jijini Addis Ababa Ethiopia, ambapo Tanzania iliwakilishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango.
Waziri huyo amesema hatua hiyo ni fursa kwa Wataalamu wa Tafsiri na Ukalimani nchini ambao katika muda mfupi tayari Watanzania 65 wamesajiliwa kupata ajira za muda na za kudumu katika Umoja wa Afrika na Kamisheni zake.
“Kiswahili kinaendelea kushamiri kwa baadhi ya Vyuo Vikuu vya nje ya Tanzania ambavyo awali havikuwa na programu za lugha hii lakini vimeanza kuingiza Kiswahili katika programu zao na tayari kuna makubaliano ya awali ya kushirikiana kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Ethiopia, Chuo Kikuu cha Port Harcourt Nigeria na Chuo Kikuu cha Joachim Chisano cha Msumbiji kufundisha Kiswahili.
Waziri Mchengerwa ameongeza kuwa juhudi za Serikali pamoja na wadau wa Kiswahili zimewezesha lugha hiyo kupitishwa rasmi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Novemba 23, 2021 na kupewa siku maalum ambapo Julai 7 ya kila mwaka imetambuliwa na kupewa heshima ya kuwa Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani.