Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako amesema Maadhimisho ya wiki ya Viziwi Duniani yatakayofanyika Septemba 25 – 30, 2023 jijini Mbeya ni kwa ajili ya watu wote na si watu wenye ulemavu wa kusikia pekee.

Ndalichako aliyasema hayo wakati akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu maadhimisho hayo yenye kauli mbiu isemayo, “Dunia Ambayo Popote Walipo Viziwi Wanaweza Kutumia Lugha ya Alama” na kuwataka wananchi kujitokeza kushiriki, kwani watapata elimu mbalimbali kuhusu masuala ya viziwi ili wawe msaada kwa watu wenye changamoto ya kutosikia au usikivu hafifu.

Amesema, “Tanzania inaungana na nchi nyingine duniani katika wiki ya Viziwi Duniani ili kutoa fursa kwa viziwi kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kushirikiana na jamii inayowazunguka bila ya kuwepo vikwazo vyovyote ikiwepo vikwazo vya mawasiliano yao.”

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako.

Maadhimisho hayo, yanakuja ikiwa ni mwendelezo wa tangu Shirikisho la Viziwi Duniani – WFD, lilipozindua Siku ya Viziwi Duniani mwaka 1958 ili kuibua changamoto zinazowakumba viziwi na namna ya kuzikabili ambapo Ndalichako pia amesisitiza juu ya matumizi ya lugha ya alama ili kuwafanya viziwi kuelewa na kushiriki katika shughuli za jamii.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania, Mhe. Bw. Ernest Kimaya ameishukuru Serikali kwa kuwajali watu wenye ulemavu nchini katika nyanja tofauti tofauti ikiwemo kuwashirikisha kwenye fursa za kiuchumi.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Viziwi Tanzania – CHAVITA, Adam Shaban aliwataka watu wote wenye ulemavu kushiriki maadhimisho ya wiki ya viziwi duniani ili kuendelea kujifunza na upata uelewa zaidi kuhusu changamoto zinazowakabili na jinsi ya kuzitatua.

Mkuu wa Majeshi atoa tahadhari ya ujio wa Vita
Makamu Rais GGML atembelea maonesho ya madini Geita